Home > All Stories > Kutoka ‘Saba Saba’ 1977 hadi ‘Nane Nane’

Kutoka ‘Saba Saba’ 1977 hadi ‘Nane Nane’

Na Daniel Mbega

NAUKUMBUKA mwaka 1978 vizuri sana, kwani wakati huo nilikuwa bado kijana mdogo, nikiwa nimetinga lubega, sime kiunoni, fimbo mkono wa kulia na mkuki mkono wa kushoto, nikichunga ng’ombe huko ‘Tanganyika’, ambako maendeleo ndiyo kwanza tulikuwa tukiyasikia kupitia Redio Tanzania (kwa wale waliokuwa na redio za mkulima) ukiwa msamiati mgeni kabisa, huku zikiwa kama simulizi ambazo hazikuwa na tofauti na zile za akina babu walizokuwa wakitupigia nyakati za jioni tukiota moto kukabiliana na baridi kali kwenye maboma yetu ya mifugo.
Zilikuwa ni simulizi kwa sababu kwetu sisi ambao tulikuwa tumehamishwa huku na huko porini ili tukaishi katika vilivyoitwa ‘Vijiji vya Ujamaa’ yalikuwa mateso makubwa kwa kuwa huko tulikopelekwa hakukuwa na huduma yoyote ya kijamii, zaidi ya kupewa ahadi nyingi kwamba tungetengenezewa barabara na huduma nyinginezo muhimu, huku wazazi wetu wakilazimishwa kushiriki katika ‘Kilimo cha Kisasa’ na kuanzisha ‘Mashamba ya Ujamaa’.
Lakini ni miezi michache kabla ya kuzuka kwa vile vita pekee ambavyo Tanzania ilipata kupigana na jirani zake, Vita vya Kagera, ambapo siku moja nikiwa nimetoka huko porini tulikokuwa tukichunga mifugo yetu na kwenda kijiji kutembea, niliposikia wimbo ukipigwa redioni ambao nakumbuka maneno machache tu yasemayo: “…Safari yetu Mbeya, tulifurahi sana. Wakazi wote wa Mbeya, walitushangilia. Sikukuu ya wakulima Saba Saba!”
Baadaye nikaja kujua kwamba kumbe wimbo huo uliimbwa na bendi moja ya ‘Wazaire’ waliokuwa wamehamia nchini Tanzania, Orchestra Marquis du Zaire (sasa haipo kwenye ulimwengu wa muziki), uliotungwa mwaka huo wa 1978 baada ya maonyesho (nadhani ya pili) ya wakulima yaliyofanyika mkoani Mbeya mwaka huo huo. Ni hapo ndipo nilipoanza kutilia maanani kuhusu sikukuu ya Saba Saba kwamba kumbe ilikuwa ni ya wakulima!
Wale vijana wa enzi zile; wasomi, waliostaarabika tofauti na siye ‘Watanganyika’ tuliokuwa tukivaa lubega, ambao walikuwa wanapenda kutinga mavazi ya ‘kisasa’ kwa wakati huo kama Bugaluu, Pekosi, taiti, tinabuu viatu vya Raizoni huku nywele zao wameziweka kwa mtindo wa Afro na wengine wameweka staili ya ‘Kambona’, wanakumbuka vizuri sherehe hizi za wakulima tofauti na vijana wa sasa wanaokulia ‘chips-mayai’.
Vijana wa sasa ukiwaeleza watakushangaa kama eti enzi zetu wakulima walikuwa wanaazimisha sikukuu ya Saba Saba tarehe saba ya mwezi wa saba, na siyo kama ilivyo sasa hivi kwamba sikukuu hiyo inaadhimishwa tarehe nane mwezi wa nane, yaani ‘Nane Nane’
Zamani ilikuwa ukitaja ‘Saba Saba’ kila mmoja anaelewa unazungumzia nini. Ukiachilia mbali sikukuu nyingine zilizozoeleka zinazoitwa za ‘mapumziko’ zaidi kwa wafanyakazi, Watanzania wa wakati ule walizitambua Saba Saba, Krismasi, Mwaka Mpya, Pasaka, na Idd (el Fitr na el Haji) ambazo kwao zilikuwa ni za sherehe kweli kweli. Hizi nyingine za Uhuru na Jamhuri, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano zilikuwa za kawaida sana kwao.
Kama ilivyo kwa sikukuu za Krismasi, Mwaka Mpya, Pasaka na Idd, Watanzania waliichukulia Saba Saba kama sikukuu adhimu kwao. Nakumbuka jinsi nilivyokuwa nikimsumbua baba yangu wakati huo kabla ya Saba Saba, kwamba lazima atununulie nguo za ‘kutokea’ kwenye sikukuu. Asipofanya hivyo ajue kesho hatuendi kuchunga ng’ombe!
Wakati ule tulisherehekea Saba Saba kwa ngoma na burudani aina kwa aina za asili, na siku hiyo kama hukupata wasaa wa kwenda kwenye ‘sikukuu’ ambako ilikuwa ni mahali pa wazi palipoandaliwa na serikali ya kijiji au mji, ama kwa kukosa nguo au nafasi, basi ungejilaumu sana kwa kukosa siku hiyo muhimu mno.
Lakini si wakati ule tu, hata sasa hivi ukipita huko vijijini, ambako huwa nalazimika kuita ‘Tanganyika’ kutokana na miundombinu duni iliyopo huko japo tumepata uhuru miaka 50 iliyopita, utakuta watu bado wanaichukulia Saba Saba kama sikukuu ya kipekee – ingawa sasa imehamishwa na kuwa Nane Nane.
Sikukuu hii ya Saba Saba ilikuwa kubwa sana si kwa sababu iliwahusu wakulima, bali ni kwa kuwa ilikuwa imerithiwa miaka mingi nyuma ikiazimishwa kila mwaka kama mojawapo ya sherehe za kitaifa zilizokuwa na nguvu. Vijana wengi wa sasa hawawezi kuelewa vizuri.
Umuhimu wa sikukuu hiyo ulitokana na ukweli kwamba yalikuwa ni maadhimisho ya kuzaliwa kwa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilicholeta Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961. Chama hiki kwa mujibu wa historia kilizaliwa pale Mtaa wa Lumumba, mahali zilipo ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuunganishwa kwa vyama viwili vya Tanganyika African Association (TAA) na African Association (AA) tarehe 7/7/1954.
TANU ndicho chama kilichotawala nchi baada ya uhuru wa Desemba 9, 1961 hadi Februari 5, 1977 kilipounganisha nguvu na chama cha Afro-Shiraz Party (ASP) cha Zanzibar na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili Tanzania itawaliwe na chama kimoja tu cha siasa baada ya nchi mbili (Tanganyika na Zanzibar) kuwa zimeungana Aprili 26, 1964. Ikumbukwe kwamba ASP nayo ilizaliwa Februari 5, 1957 kama ilivyokuwa kwa Azimio la Arusha lililohimiza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ambalo lilizaliwa Februari 5, 1967.
Kwa hiyo utaona kwamba kwa miaka takriban 15 (1961 – 1976) Watanzania Bara walikuwa wakiendelea kusherehekea kuzaliwa kwa TANU kila tarehe saba ya mwezi Julai, lakini mara tu baada ya kuzaliwa kwa CCM ikabidi sherehe za Saba Saba zibadilishwe na kuitwa ‘Sikukuu ya Wakulima’, lengo likiwa ni kuhimiza sera ya serikali kwa wakati huo ya ‘Siasa ni Kilimo’.
Saba Saba ya miaka hiyo ilikuwa na maana halisi ya kuhimiza ‘Siasa ni Kilimo’, kwa sababu katika maonyesho ya kiwilaya, kimkoa na kitaifa, wakulima walionyesha mazao halisi ya kilimo, wakaonyeshwa pembejeo za kilimo ‘cha kisasa’ na kufundishwa namna ya kutumia pembejeo hizo kwa ustawi wa kilimo na taifa kwa ujumla.
Mjini Dar es Salaam sikukuu hii ilitengewa eneo lake maalum katika Barabara ya Kilwa, ambalo lipo mpaka leo, na huko mikoani kulijengwa viwanja maalum kwa ajili ya maonyesho hayo, watu wakiingia bure kuangalia bidhaa na mazao ya kilimo pamoja na kuangalia pembejeo na kujifunza matumizi yake.
Kadiri miaka ilivyozidi kusonga mbele, dhana ya ‘Siasa ni Kilimo’ kilibadilika na kuwa ‘Siasa ya Kilimo’ na wengine wakaitafsiri kama ‘Kilimo cha Siasa’, kwa sababu sikukuu hiyo ilionekana kujaa siasa zaidi, huku watu wakilenga kuitumia kibiashara kuliko maazimio ya awali.
Haikushangaza hata hivyo katikati ya miaka ya 1990 wakati serikali ilipoamua kuwahamisha wakulima kutoka ‘Saba Saba’ na kuwapeleka katika siku nyingine ya ‘Nane Nane’. Lengo la serikali sasa likawa kuitumia Saba Saba kama siku ya maonyesho ya biashara ya kimataifa, ambapo wafanyabiashara wengi walijitokeza ama hujitokeza kuonyesha bidhaa zao wanazozalisha na siyo kuwafundisha Watanzania mbinu za kuzalisha biadhaa hizo.
Saba Saba imekuwa siku ya kibiashara kwa sababu katika eneo lile la Kilwa Road, kwenye viwanja vilivyobatizwa jina la Mwalimu Nyerere, ambako watu walizowea kuingia bure kununua mahitaji yao kwa bei nafuu tofauti na mahali pengine, leo hii mtu mzima huwezi kuingia bila kulipia shilingi 2,000. Na uwapo ndani usitegemee kukuta bidhaa za bei nafuu, bali bei zake ni za juu mno kuliko hata ukizinunua bidhaa hizo hizo kwa Wamachinga. Kisa? Watakwambia wao wanalipia mabanda hayo kwa bei kubwa, hivyo lazima wafidia gharama!
Awali sikukuu ya Nane Nane ilianza kwa kupooza katika maonyesho ya kwanza yaliyofanyika mjini Morogoro katika eneo la Nane Nane, lakini sasa hali inaonekana kuwa tofauti kidogo. Maonyesho hayo ambayo yamefanyika sehemu mbalimbali nchini kitaifa kama Arusha kwenye viwanja vya Kemi na TASO, Mbeya, Mwanza na Dodoma, yameanza kuvutia wengi, lakini kama kawaida, wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara zaidi wa kilimo.
Ni wafanyabiashara wa kilimo kwa sababu wanapeleka bidhaa ‘zinazofanana’ na za kilimo, baadhi yake zikiwa siyo halisi. Unawezaje kupeleka kwenye maonyesho haya maua ya bandia? Kama suala ni kuhimiza kilimo cha maua, kwa nini watu wasipeleke maua halisi na utaalamu wa kulima maua hayo badala ya kufikiria kuuza bidhaa zao tu?
Kitaifa maonyesho hayo ya mwaka huu yamefanyika pia mkoani Dodoma, lakini wakulima wengi wenzangu na mimi wametoka vichwa chini kwa sababu pembejeo zinazoonyeshwa huko zinauzwa aghali kiasi kwamba mkulima huyu wa kawaida anayetafuta namna ya kujikwamua na jembe la mkono hawezi kumudu.
Serikali inaendelea kusisitiza mbolea za chumvi chumvi kwa wakulima, lakini mbolea hiyo ya ruzuku inapatikana kwa bei ya juu mno, mfuko mmoja ukiuzwa hadi shilingi 120,000. Mkulima mwenye eneo la ekari 10 atatakiwa awe na zaidi ya shilingi milioni moja ili aweze kupata mbolea peke yake, achilia mbali gharama za kukodisha trekta na pembejeo nyingine kama mbegu bora, madawa na kadhalika.
Pia katika sehemu nyingi, mbolea hizo za chumvi chumvi zimeonekana kuharibu ardhi, kwani zikitumiwa kwa muda mrefu zinatengeneza sumu ambayo inafanya ardhi hiyo izeeke na hivyo kuwalazimu wakulima watafute sehemu nyingine zaidi kupata ardhi ya kilimo. Mwisho wa siku misitu mingi inavamiwa na kufyekwa, na baada ya miaka kadhaa nchi inakuwa jangwa huku migogoro mingi ya ardhi ikiibuka.
Maonyesho haya ni vyema yakatumiwa na serikali kwa kupeleka wataalamu wa ugani ambao watawahamasisha wakulima kutumia mbolea ya mboji ya asili, isiyo na kemikali, ili kurutubisha ardhi na kuwafanya wawe na kilimo endelevu badala ya mbolea za chumvi chumvi, ambazo zinazeesha udongo na pia ni ghali.
Kama kweli maonyesho ya Nane Nane tunataka yabebe ujumbe unaostahili, serikali inatakiwa kuwawekea wakulima, hasa wadogo wadogo, mazingira bora zaidi ya kuonyesha mazao yao ya kilimo na kuwatafutia masoko ili waweze kujikomboa.
Ingawa serikali imeongeza fungu la bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012, huku ikiwa na kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’, dhamira yake nzuri inaweza isitimie ikiwa jitihada za dhati hazitakuwepo katika kuhakikisha wakulima wanajengewa mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao.
Kama ‘Siasa ni Kilimo’ ilibadilishwa na kuwa ‘Kilimo cha Siasa’ au ‘Siasa ya Kilimo’, nadhani kuna haja kwa serikali na wadau wote kuketi chini kutafakari wapi tulipojikwaa kabla ya kuanza utekelezaji wa ‘Kilimo Kwanza’, vinginevyo tutaletewa msamiati mwingine wa ‘Siasa Kwanza, ndipo Kilimo’!

Nipigie: +255-715-070109, +255-783-130109, au e-mail: mbega.daniel@gmail.com
Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: