Home > All Stories > RIPOTI MAALUM MBARALI

RIPOTI MAALUM MBARALI

‘Tuko tayari kufa kwa risasi’

Mzee Andrew Mlali mkazi wa Ubaruku akionyesha alama iliyochongwa na mwekezaji kama mpaka wake katikati ya mashamba ya wakulima.

Na Daniel Mbega, Mbarali

MGOGORO wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji saba vinavyozunguka shamba la mpunga la Mbarali na mwekezaji umechukua sura mpya wiki hii baada ya wananchi kutamka bayana kwamba wako tayari kufa kwa risasi kupigania ardhi yao.

Wananchi hao wametoa kauli hiyo baada ya mwekezaji huyo, kampuni ya Highland Estate Limited, kuvamia mashamba yao katika kijiji cha Urunda, Kata ya Imalilo-Songwe, wilayani hapa Jumatano iliyopita na kuanza kuyapima kwa nia ya kuwakodishia wakulima wengine wasio wakazi wa vijiji hivyo.

“Tuko tayari kufa kwa risasi, lakini siyo kwa njaa. Tutayapigania mashamba yetu kwa nguvu zetu zote, hatuko tayari kuona tunanyanyasika kwa kuporwa ardhi yetu ambayo tumekuwa tukiilima kwa takribani miaka 40 sasa,” wananchi hao walisikika wakisema mbele ya Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, aliyefika eneo la tukio na kuwaasa wasitumie nguvu.

Wananchi hao walifikia hatua hiyo kujitoa muhanga baada ya mwekezaji huyo kutuma maofisa wake walioambatana na mgambo wenye bunduki na kuanza kupima takribani ekari 400 za wananchi kijijini hapo anazodai ziko kwenye eneo lake.

Mbali ya kwenda na mgambo wenye silaha, mwekezaji huyo aliamua kupiga simu kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya akiomba msaada wa askari kwa maelezo kwamba kulikuwa na vurugu, ambapo OCD alituma kikosi cha askari wenye silaha bila hata kujua vurugu hizo zilihusu ama zilitokana na nini.

Mbunge aepusha umwagaji damu
Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, ambaye alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya askari hao kufika, anasema alitumia muda mwingi kuwatuliza wananchi hao wasifanye fujo huku akiwasiliana na uongozi wa wilaya.

“Mkuu wa Wilaya alikuwa kwenye kikao mjini Mbeya, lakini nilipomuuliza OCD kwa nini aliwatuma askari bila kujua tatizo ni nini, alisema yeye alikwenda kutuliza fujo, lakini akakubali kuwarudisha askari hao,” alisema Kilufi.

Hata hivyo, baada ya askari hao kuondoka, mgambo waliopelekwa na mwekezaji walianza kufyatua risasi hewani kuwatishia wananchi, hatua ambayo inadaiwa kuwapandisha hasira wananchi hao na kumweleza Mbunge kwamba wako tayari kufa lakini wasingeruhusu upimaji wa mashamba yao uendelee.

Kwa mtazamo wake, Kilufi alisema, kinachoonekana ni tamaa ya kibepari ya mwekezaji ambaye ameshindwa kuliendeleza shamba alilouziwa ambapo amekuwa akilikodisha kwa wananchi miaka yote hiyo na sasa anataka kuvamia na kwa wananchi.

“Shamba lake tu mwenyewe analima hekta chache sana, sehemu kubwa anaikodisha na kwingineko limemshinda kabisa amefanya malisho ya mifugo. Sasa inakuwaje avamie na mashamba ya wananchi yaliyoko pembezoni?” alihoji Kilufi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Anaclet Malimbisa, amekiri kutokea kwa tukio hilo na akampongeza Mbunge wa Mbarali kwa kufanikiwa kutuliza ghasia.

Hata hivyo, alisema suala hilo linashughulikiwa na amempa maelekezo OCD kulishughulikia kwa busara ili kudumisha amani na usalama wilayani humo.

“Ninazo taarifa za tukio hilo la Jumatano, lakini nimeshatoa maelekezo kwa OCD ambao kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya watayashughulikia,” alisema. “Namshukuru Mbunge kwa kuwashauri wananchi wasifanye fujo.”

Mkuu wa Wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali (mstaafu) Cosmas Kayombo, alisema kwa nyakati tofauti amekutana na wawakilishi wa wakulima wa Urunda na mwekezaji na kuzungumza nao kwamba suala hilo liko ngazi ya Mkoa na litashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu, hivyo wawe wavumilivu.

DC Kayombo alisema hata hivyo kuwa, amemtaka mwekezaji asiendelee na zoezi la upimaji na kwamba wananchi nao wasifanye shughuli zao kwenye eneo hilo la mgogoro hadi hapo Mkuu mpya wa Mkoa, Abbas Kandoro, atakaporipoti kazini na kupewa taarifa kamili ili atoe maelekezo kabla ya msimu wa kilimo kuanza.

“Tatizo lile limekuwa likishughulikiwa na linahusisha mipaka. Halmashauri ya Wilaya tumelishughulikia kwa kirefu na tumepeleka mapendekezo yetu ngazi za juu tangu mwishoni mwa mwaka jana, naamini yatafanyiwa kazi,” alisema.

Wananchi waonya
Kundi la wananchi 30 lilivamia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Alhamisi asubuhi na kufanya kikao cha takribani saa moja, ambapo wengi wao walisema wana mashaka kuhusu namna suala hilo linavyoshughulikiwa.

Wakizungumza baada ya kuonana na Mkuu wa Wilaya, wananchi hao walisema kwamba serikali inafanya masihara na uhai na uchumi wao kwa kushindwa kulitatua haraka suala hilo, hali ambayo inaleta harufu ya damu kwenye eneo hilo.

“Uzembe wa serikali ndio kwa kiasi kikubwa ulisababisha kifo cha mwananchi mmoja Januari 13 mwaka huu baada ya kupigwa risasi na polisi, sasa tena mwekezaji huyu huyu anayekimbilia kutumia dola ameanza na serikali haitaki kutamka wazi nini kifanyike. Matokeo yake wananchi watachoka na kitakachofuata ni kushuhudia umwagaji damu,” alisema Dafeti Hussein.

Hussein (51) ambaye ni mzaliwa wa eneo hilo, alisema uchumi wao unategemea kilimo na kwa miaka yote wamekuwa wakilima mashamba hayo huku wakitambua kwamba mwisho wa shamba la mwekezaji ni kwenye tuta kubwa la mfereji, lakini sasa wanashangaa ni kwa vipi amevamia mashamba yao na kutaka kuyakodisha kwa wengine.

Aliongeza kwamba, mashamba wanayolima wamekuwa wakiyatumia tangu mwaka 1974 baada ya kuupisha mradi wa shamba hilo, ambapo maeneo hayo yalikuwa mapori na yakafyekwa na wazazi wao.

Naye Rogers Kidasi (35) mkazi wa kijiji hicho cha Urunda, alisema kwamba wako tayari kuuawa kwa risasi lakini si kushuhudia familia zao zinakufa kwa njaa kwa sababu ya mwekezaji.

Kidasi alisema tangu anazaliwa amekuta wazazi wake wakilima mashamba hayohayo tangu mradi wa shamba Mbarali Estate lenye ukubwa wa takribani hekta 6,030 ukimilikiwa na Wachina na baadaye NAFCO.

Diwani wa Kata ya Imalilo-Songwe, George Chaula, aliyeongozana na wakulima hao kwa Mkuu wa Wilaya, alisema kwamba anasubiri kauli ya mwisho ya DC baada ya kuwasiliana na uongozi wa mkoa ili kudumisha amani kwenye eneo hilo na kuwaacha wananchi waendelee na kilimo ili kukuza uchumi wao.

Mwekezaji mwenyewe ameshindwa kupatikana hata kwa njia ya simu ili kuzungumzia sakata hilo, ingawa DC alisema tayari ameshasitisha zoezi hilo.

Alama iliyowekwa na mwekezaji kama mpaka wa shamba lake. Hapa ndipo risasi ziliporindima Jumatano iliyopita.

Mfereji mkuu wa Maji ambao unaelezwa kuwa ndio mpaka baina ya mwekezaji na wananchi tangu enzi za NAFCO.

Mfereji mkuu wa maji ambao wananchi wanasema ndio mpaka wa shamba la mwekezaji tangu likiwa chini ya NAFCO.

Mpaka uliochongwa na mwekezaji tangu mwaka 2010.

Baadhi ya nyumba za wakazi wa kijiji cha Urunda jirani na shamba la mwekezaji

Ofisi Kuu ya Highland Estates Limited kwenye shamba la Mbarali.

Ofisi kuu ya Shamba la Mpunga Mbarali ilipo na mashine ya ukoboaji.

Shamba la mwekezaji ambalo amekodisha wananchi.

Wananchi waliokodisha mashamba ndani ya Mbarali Estate wakiwa wamekwishaanza kulima kwa msimu ujao.

Zahanati iliyokuwa ikitumiwa na wananchi ambayo ilibomolewa na mwekezaji baada ya kununua shamba hilo mwaka 2006. (PICHA ZOTE ZA DANIEL MBEGA).

 

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. Charlesi Chinamani
    October 2, 2015 at 3:19 pm

    Wana Inchi Wa Ubaruku Mm Nawajua Watata Sana Kwa Iyo Mwekezaji Awe Nao Kalibu Asiwaingilie Kwenye Maeneo Yao Iyo Itakuwa Ubepali Wa Wazee Wetu Wa Zamani

  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: