Home > All Stories > Kapunga sasa kujengewa kituo cha afya

Kapunga sasa kujengewa kituo cha afya

Na Daniel Mbega

SERIKALI wilayani Mbarali, mkoani Mbeya inakusudia kujenga kituo cha afya katika kijiji cha Kapunga ikiwa ni harakati za kuwanusuru na shida kubwa ya ukosefu wa huduma za afya.
Taarifa za uhakika zinaeleza kwamba, tayari uongozi wa halmashauri hiyo umekwishawasilisha michoro ya kituo hicho ambacho kitawaokoa hasa wajawazito, watoto na wazee wanaotembea zaidi ya kilometa 50 kufuata tiba.
“Tumeletewa michoro, lakini tunawasubiri viongozi wa wilaya waje tuwaonyeshe mahali ambako tunataka kituo hicho kijengwe,” amesema mwenyekiti wa kijiji hicho, Ramadhan Nyoni.
Michoro hiyo, ambayo Mwananchi limefanikiwa kupata nakala yake, imetengenezwa na kampuni ya Mecon Arch Consult Limited ya jijini Dar es Salaam, ambayo ndiyo iliyoingia mkataba na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya michoro ya vituo vya afya.
Nyoni amesema hata hivyo kwamba, hawajafahamu ujenzi wa kituo hicho utagharimu kiasi gani, isipokuwa anaamini kwamba gharama kubwa zitabebwa na halmashauri na wananchi wanaweza kuchangia asilimia fulani.
Kwa zaidi ya miaka sita sasa wananchi wa Kapunga na vijiji vya jirani wamekuwa wakitembea zaidi ya kilometa 50 kwenda na kurudi Chimala kufuata matibabu.
Hatua hiyo imetokana na kufungwa kwa zahanati waliyokuwa wakiitumia kwa takriban miaka 15 baada ya serikali kuuza lililokuwa Shamba la Mpunga la NAFCO kwa mwekezaji, Kampuni ya Export Trading Limited mwaka 2006.
Mwekezaji huyo aliamua kubadilisha matumizi ya majengo mengi baaa ya kukabidhiwa, ingawa zahanati hiyo imetelekezwa tangu wakati huo bila huduma zozote.
“Tunatembea kilometa 58 kwenda na kurudi Chimala kufuata tiba, hata kama ni malaria. Akinamama wajawazito, watoto na wazee ndio wako kwenye mateso makubwa, kwani hakuna huduma hapa na gharama za usafiri kwa kipato chetu wengi hatuzimudu,” anasema Emanuel Kasekwa (35) mkazi wa kijiji hicho.
Naye Mbuke Sena (36), mama mjamzito na mkazi wa kijiji cha Mbalino, anasema kujengwa kwa kituo cha afya kijijini Kapunga kutawanusuru wanawake wengi wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya ya uzazi.
“Ninatoka kliniki umbali wa kilometa 30 hadi Chimala kwa kutumia baiskeli. Nimewahi kuharibu mimba mara mbili kutokana na mikiki mikiki ya safari hizi. Serikali itafanya jambo la maana sana kutujengea kituo cha afya,” anasema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, George Kagomba, hakuweza kupatikana kuzungumzia ujenzi huo, lakini ofisa mmoja wa idara ya afya wilayani humo amekiri kwamba eneo la Kapunga na vijiji vya jirani havijapata “huduma bora” za afya na halmashauri inafanya jitihada za kuwapatia wananchi huduma hizo.

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: