Home > All Stories > Kilimo cha umwagiliaji chaondoa njaa Songea

Kilimo cha umwagiliaji chaondoa njaa Songea

Na Daniel Mbega, Songea

ISAAC Luena (57), mkulima mdogo katika kijiji cha Namatuhi wilayani Songea, sasa anashuhudia kuongezeka maradufu kwa mavuno yake. Haya ni matunda ya program ya umagiliaji inayofadhiliwa na serikali.

Idara ya Kilimo Wilaya ya Songea imekuwa ikiwapatia wakulima wadogo mbegu bora, mafunzo na ushauri wa mbinu za kilimo, mpango ambao umeleta matunda mazuri.

“Kabla ya kuboresha mpango huu wa umwagiliaji mwaka 2008, tulifanya kazi kwa nguvu na kupata mavuno kidogo – kama tani 1.5 kwa hekta moja ya mpunga. Lakini serikali ilipoanza kutusaidia, taswira nzima ya uzalishaji ikabadilika. Kila mwaka tangu 2008, tumekuwa tukivuna tani nne mpaka tano kwa hekta moja ya mpunga aina ya IR 64,” anasema Luena.

Kwa mavuno hayo, Luena anasema, sasa anaweza kuuza sehemu ya mpunga na kuwasomesha watoto wake watatu sekondari na kubakiwa na ziada ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani.

Anaongeza kwamba, kwa sasa wanaweza kuzalisha mara mbili kwa mwaka tofauti na zamani walipokuwa wakitegemea mvua za masika pekee.

Luena ni miongoni mwa wakulima 2,268 wanaonufaika na Skimu ya Umwagiliaji Namatuhi yenye ukubwa wa eneo la hekta 220 katika Mto Masimeli unaotiririsha maji yake kwenye Mto Ruvuma.

Skimu hiyo ilianzishwa mapema mwaka 2001 kwa maendeleo ya jamii ambapo wakulima walikuwa wakitumia kilimo cha asili ambacho kilionekana kukosa tija kwani mavuno yalikuwa kiasi cha tani 1.5 kwa hekta kwa mbegu za mpunga aina ya Super India.

“Mwaka 2008 serikali ya wilaya ikaanza kuwapatia wakulima mafunzo katika Chuo cha Kilimanjaro Agriculture Training Centre kwa mpango wa mkulima kwa mkulima. Tulianza kuwapa mafunzo wakulima ili iwe rahisi kwao kuwafunza wengine pindi wanaporejea, mbinu hii imezaa matunda kwani wote wameachana na kilimo cha asili cha kumwga mbegu tu na kutegemea mvua,” anasema Mhandisi Jerome Mponela, ofisa umwagiliaji katika Idara ya Kilimo wilayani Songea.

Mponela anasema wakulima walifunzwa namna ya kutumia majaruba badala ya kumwaga mbegu holela, na wakapatiwa aina tofauti za mbegu za mpunga kama IR 54, PSB 28, na IR 64, ambayo ilionekana kustahimili mazingira ya Ruvuma.

“IR 64 ndiyo mbegu bora kama ilivyo kwa mpunga unaozalishwa Kyela. Wastani wa mavuno hasa kwa Skimu ya Umwagiliaji Namatuhi ni tani tano kwa hekta,” anasema.

Anasema, Skimu ya Namatuhi, ambayo awali ilikadiriwa kugharimu Shs. 560 milioni mwaka 2001, bado miundombinu yake haijakamilika na gharama zinazidi kupanda ambapo sasa wanahitaji Shs. 400 milioni ili kuhakikisha mfereji wenye urefu wa kilometa 6 unajengwa pamoja na maingilio kwenda kwenye mashamba.

Mponela anaeleza kwamba Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeahidi kutoa ruzuku ya Dola za Marekani 200,000 kama sehemu ya kuendeleza Bonde la Mto Ruvuma, wakati ambapo wamepatiwa pia Shs. 200 milioni kutoka Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Umwagiliaji (NIDF) ili kuhakikisha miradi ya umwagiliaji wilayani humo inakuwa ya kudumu.

Kusaidia miradi ya kilimo na usalama wa chakula hasa kwa nchi zinazoendelea ni miongoni mwa mada zinazojadiliwa kila wakati katika majukwaa ya kimataifa.

Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) unahimiza kilimo cha wakulima wadogo kama fursa pekee kwa watu wa vijijini wanaohuisha ukuaji wa masoko ya chakula katika miji mikubwa ya nchi zinazoendelea.

Usalama wa chakula

Idadi kubwa ya wakazi wa wilaya ya Songea kwa miaka mingi imekuwa ikikumbwa na uhaba wa chakula, pamoja na mazingira mazuri ya kilimo. Hii inatokana na ukosefu wa mbinu bora za kilimo.

Ni kutokana na changamoto hiyo ndiyo maana serikali ya wilaya ikaamua kuanzia skimu za umwagiliaji, matunda yaliyobadilika kutoka uzalishaji wa chakula pekee hadi kuwa biashara.

Mponela anasema, program za umwagiliaji sasa zinaendeshwa wilayani humo ambapo kwa sasa kuna skimu 34 kama Namatuhi, Mpitimbi (A na B), Muhukuru, Lilahi na Nakahuga zote zikiwa na ukubwa wa hekta 823.

“Jumla ya hekta 13,399 zimeainishwa kama maeneo yanayofaa kwa umwagiiaji lakini kwa sasa tuna eneo la hekta 4,700 linalotumika kwa umwagiliaji. Changamoto kubwa inayotukabili ni fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji,” anaongeza Mponela.

Ofisa Kilimo wa Wilaya, Maswaga, anasema changamoto inayowakabili katika uzalishaji wa mpunga ni miundombinu duni, wadudu na magonjwa ya mpunga kama viwavi jeshi, kuoza kwa shina na kupauka.

“Serikali inajenga barabara na kuanzisha masoko kwa wakulima kuuza mazao yao wakati tunaendelea kutafuta fedha za kutosha kujenga mifereji ya umwagiliaji katika skimu nane yenye urefu wa kilometa 13,” anasema Maswaga.

Maswaga anasema, program ya umwagiliaji inahusisha mambo makuu manne: msaada wa kitaasisi, kujengewa uwezo, kuwezesha uzalishaji wa kilimo, na ukarabati wa miundombinu ya kichumi na kijamii.

“Mara mbili kwa mwaka huwapa mafunzo wakulima wadogo kwa kuwapeleka KATC mjini Moshi. Wanapewa mbegu bora nasi tunasimamia, japo si mara kwa mara kutokana na ufinyu wa bajeti,” anasema.

Kwa mujibu wa Maswaga, mbegu bora za mpunga zina muda mfupi na mavuno yake ni makubwa na pia zinastahimili magonjwa ya mimea kulinganisha na mbegu za asili.

“Kwa sasa, zaidi ya kaya 50,000 zinanufaika na mazao bora ya kilimo. Na zaidi ya kilometa 150 za barabara zimekarabatiwa kuwawezesha wakulima wadogo kupeleka mazao yao sokoni,” anaongeza.

Advertisements
Categories: All Stories
  1. odeni herodi
    December 21, 2015 at 5:31 am

    je sehemu zenye milima kilimo cha umwagiliaji inawezekaneje au njia gan inatumika kutatua Hilo

  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: