Home > All Stories > Ni gharama kubwa kubeba mimba Kapunga

Ni gharama kubwa kubeba mimba Kapunga

Na Daniel Mbega, Mbarali

KATIKA daraja dogo lililowekwa magogo likiunganisha vijiji vya Kapunga na Mbalino, wilayani Mbarali, Yohana Siling’wa (38) anakokota baiskeli akiwa amembeba mkewe Mbuke Sena (32) ambaye ni mjamzito. Wanarejea kutoka kliniki ya kila mwezi katika Hospitali ya Misheni Chimala, yapata umbali wa kilometa 29 kutoka kijijini kwao Mbalino.

Ni jua la utosini na Siling’wa anatoka jasho kweli. Ni kazi ngumu kuendesha baiskeli kutoka Mbalino hadi Chimala na kurejea katika wakati huu wa jua kali, na hasa unapokuwa umembeba mtu mwenye hali kama ya Sena. Njia ni mbaya mno.

Msamaria mwema anawasaidia kuwasukuma hadi ng’ambo ya daraja la mfereji huu wa kumwagilia maji kwenye mashamba ya mpunga.

“Walau nitapumzika kwa mwezi mmoja kabla ya kumrejesha tena kliniki kwa ajili ya kujifungua. Safari ya kuendesha baiskeli kwa kilometa 58 kila wakati aendapo kliniki inachosha mno. Nadhani huu utakuwa ujauzito wake wa mwisho,” anasema Siling’wa.

Anaeleza kwamba ingawa wana watoto sita, huu ni ujauzito wake wa kumi. Sena amewahi kuharibu mimba mara mbili na mwaka jana, wawili hao walipoteza binti yao wa miaka mitanoi kutokana na malaria kali.

“Ni kazi ngumu, lakini nimezowea kumpeleka mke wangu kiliniki kila mwezi. Watoto wangu wanne walizaliwa katika Hospitali ya Misheni Chimala. Nimekuwa nikikabiliana na hali hii kila wakati mke wangu anapokuwa mjamzito na sasa nasema imetosha,” anasema.

Ikiwa imejengwa Chimala kando ya barabara kuu ya Dar es Salaam – Mbeya, Hospitali hii ya Misheni, ambayo ilijengwa tangu mwaka 1962 na wamisionari wa Kanisa la Kristo la New York Arena, inatoa huduma kwa watu zaidi ya 25,000, kwa mujibu wa ofisa wa kituo hicho. Iko umbali wa kilometa 30 kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mbarali mjini Rujewa.

Lakini Sena anakumbuka kwamba ameambiwa na daktari ni kwa sababu ya mtikisiko wa baiskeli ndiyo maana akaharibu mimba mara mbili.

“Afadhali sasa, lakini wakati ule njia ilikuwa mbovu mno na hatuna namna yoyote ya usafiri kutoka kijijini kwetu, ambako ni kilometa 3 kutoka Kapunga, kwani njia hazipitiki kutokana na miundombinu duni. Kama kungekuwepo na zahanati Kapunga ingekuwa rahisi kwangu kutembea na kuhudhuria kliniki,” anasema.

Hata hivyo, anasema hawana fedha za nauli ya daladala kutoka Kapunga hadi Chimala ambapo gharama yake ni Sh. 8,000 kwa watu wawili, hivyo ni rahisi kwao kutumia baiskeli japokuwa ni hatari kwa hali yake.

“Kila ninaporejea nyumbani, mgongo na kiuno vinaniuma hadi nalazimika kumeza vidonge vya maumivu ili nilale,” anaongeza.

Mtoto wao wa kwanza, Luhunga, ana miaka 14 na yuko darasa la sita, wakati mtoto wa mwisho, Stella, ana miaka miwili na nusu.

Kwa vile wanaishi mbali, daktari katika hospitali ya misheni amewashauri wakapange chumba Chimala wiki tatu kabla ya Sena kujifungua ili kupunguza usumbufu.

Hospitali hiyo inapangisha vyumba kwa Sh. 500 kwa mtu mmoja, kwa usiku mmoja, kiwango ambacho ni kikubwa sana kwa wakazi wengi wa Kapunga, ambao wanategemea zaidi kilimo kuendesha maisha yao.

“Kiasi hiki hakihusishi chakula na gharama nyingine. Na ninalazimika kuongozana na mtu mwingine atakayenihudumia. Pia ninapaswa kulipa si chini ya Sh. 35,000 kama gharama za kujifungulia. Ni tabu mno kuwa mjamzito vijijini kwetu kwa kuwa huduma za uzazi hazipatikani,” anasema Sena.

Ni tabu sana pia kuugua ikiwa unaishi Kapunga. Wanakijiji wengi wanaitegemea Hosptali ya Misheni Chimala kwa huduma za afya, kwa kuwa hakuna zahanati katika maeneo ya jirani.

“Zahanati ambayo zamani iliwahudumia wanakijiji wa Kapunga na vijiji jirani iliyokuwa katika eneo la Shamba la Mpunga Kapunga ilifungwa kitambo na mwekezaji. Sasa, hata kama unaumwa malaria unatakiwa kwenda Chimala,” analalamika Sena.

Mwekezaji katika shamba hilo, Kapunga Rice Project Limited, aliifunga zahanati hiyo ya umma mwaka 2006 baada ya kununua shamba hilo kutoka serikalini, hivyo kuwanyima maelfu ya wananchi fursa ya huduma ya afya.

Mara ya mwisho kwa zahanati hiyo kuwa na mhudumu ilikuwa miaka minne iliyopita wakati Dk. Simbili alipowasili hapo lakini inaelezwa kwamba alikaa kwa mwezi mmoja tu na kuondoka kutokana na sababu ambazo hazijawekwa wazi hadi sasa.

“Watu wanatembea zaidi ya kilometa 25 kufuata huduma ya afya na ni umbali mrefu mno, hasa kwa wanawake, watoto na wazee,” anasema mwenyekiti wa kijiji cha Kapunga, Ramadhan Nyoni.

Kibaya zaidi, wakati wa masika, barabara ya kwenda Chimala huwa haipitiki. Njia nyingine mbadala ya mzunguko ina urefu wa kilometa 40.

“Ugonjwa wa malaria ni hatari sana wakati wa masika. Na serikali kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wajawazito ni ukiukaji wa haki ya kuishi,” anaongeza Nyoni.

Kwa akina mama wengi wa Tanzania, suala la uzazi limeendelea kuwa la hatari zaidi na hata kusababisha vifo – kwa mama na mtoto na kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika la Idadi ya Watu (UNFPA) ya mwaka 2003, Tanzania ilikuwa na vifo vya uzazi 1,500 na ya sita duniani kwa idadi kubwa ya vifo ikiwa nyuma ya Sierra Leone (2,000), Afghanistan (1,900), Malawi (1,800), Angola (1,700) na Niger (1,600).

Mwanahamisi Ally (52) ni mama wa watoto wanne na mkazi wa Kapunga ambaye anasema wanawake wengi wanaamua kujifungulia nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa huduma za afya kwenye eneo hilo na umaskini kwani wanapaswa kukodisha gari kwa Sh. 40,000 kila wanapohitaji kupelekwa hospitali kujifungua.

“Sidhani kama kuna mwanamke anayeweza kukataa kujifungulia hospitali kama huduma zote zipo na zinatolewa bure. Wanawake wengi hawataki kwenda hospitali kwa sababu hakuna huduma. Na kama kuna dawa, wanatakiwa kulipia,” anasema.

Kwa Nhibula Mwasamaki (43) mama wa watoto watano, Hospitali ya Misheni Chimala imekuwa mkombozi wa wengi kwani ndicho kituo pekee cha afya wanachokitegemea ingawa wanapaswa kulipia gharama ikilinganishwa na hospitali za serikali ambako huduma ni za bure.

“Watoto wangu watatu nilijifungulia pale. Huduma ni nzuri kama si za kuridhisha,” anaongeza.

Bernard Kulanga, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Misheni Chimala, anasema ingawa kuna zahanati nyingine kwenye mji huo mdogo, kituo chao ndicho kinachotegemewa na wengi hasa kwa afya ya uzazi.

“Tunapokea wagonjwa wengi kila mara, hata wanaoumwa malaria. Watu wanakuja hapa kutokana na ubora wa huduma zetu, na kama kituo cha misheni kilicho chini ya Kanisa la Kristo, wajibu wetu ni kuhudumia  watu, hasa wanawake na watoto ambao ndio idadi kubwa ya wateja wetu,” anasema.

Kulanga anasema, hospitali hiyo, ambayo inapokea pia wagonjwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mbarali, ina watumishi 103 – Waganga watano, waganga wasaidizi wawili, Maofisa wauguzi wanne, Wauguzi 30 na watumishi wengine, japokuwa mahitaji bado makubwa.

Anasema wanapokea wastani wa wagonjwa 90 kwa siku wakiwemo wanaolazwa na wale wanaotibiwa na kuondoka. Magonjwa yanayosumbua zaidi ni malaria kali na kuhara kwa watoto.

“Kwa sababu watumishi wetu wanapaswa kulipwa, tunatoza gharama kidogo ili kuongeza kipato. Kwa wanaojifungua, hatutozi chini ya Sh. 35,000 kama wanajifungua kwa njia ya kawaida na Sh. 150,000 kwa wanaofanyiwa upasuaji. Gharama hizi zinahusisha huduma zote za tiba ikiwa ni pamoja na dawa,” anasema.

Kwa mujibu wa Kulanga, wagonjwa hulazwa kwanza na kupatiwa huduma zote bila malipo, hivyo kumwezesha kila mmoja kupata huduma za afya kwa wakati.

“Hatuwatozi gharama kabla ya tiba, sivyo tunavyofanya kazi. Tunaamini kwamba mgonjwa anahitaji tiba na malipo yatafuata baadaye. Kwa wale ambao hawana fedha huwaruhusu waende kisha waje walipe baada ya kupata fedha. Lakini wengi wao hutokomea, na hatuwezi kwenda kuwasaka mitaani,” anaongeza.

Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 1990 imelenga kuboresha huduma za afya kwa watu wote mahali walipo, mijini na vijijini, kwa kupunguza hatari na vifo na kuongeza matumaini ya maisha kwa sababu uimara wa mwili, akili na kijamii ni rasilimali kubwa kwa maendeleo ya uchumi.

Vilevile, sera hiyo imelenga kupunguza vifo vya watoto na vifo vya akina mama kabla, wakati na baada ya kujifungua kwa kuongeza huduma bora na muhimu za afya ya mama na mtoto, kuhamasisha lishe bora, kuzuia na kutibu magonjwa yanayotibika.

George Kagomba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, anakiri kwamba eneo la Kapunga na vijiji vya jirani havijapata “huduma bora” za afya.

Anasema kufungwa kwa zahanati ya umma katika lililokuwa shamba la NAFCO ni mojawapo ya changamoto zinazoikabili idara la afya kwenye halmashauri yake.

“Dira ya serikali ni kuona kila kijiji kinapata kituo cha afya na kilio cha watu hao (kutoka Kapunga) ni cha msingi sana ambacho halmashauri yangu itakishughulikia,” anasema.

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: