Home > All Stories > Nyuki wamebadili maisha yangu

Nyuki wamebadili maisha yangu

Na Daniel Mbega, Dodoma

MIAKA mitatu iliyopita Ellen Sangula (35), mkazi wa kijiji cha Ilindi wilayani Bahi, hakuwa na ndoto za kumiliki TShs. 200,000, lakini sasa kiwango hicho ni cha kawaida kwake baada ya kujiingiza katika ufugaji wa nyuki.
Matunda ya ufugaji huo wa nyuki yamemwezesha kujipatia fedha za kutosha ambazo zimemfanya aanzishe mradi wa kuku, bata na kanga ambapo kwa sasa mtaji wake unafikia TShs. 700,000.

Ellen Sangula akiwa kwenye banda lake la Bata.

Japokuwa ni kazi ngumu kufuga wadudu hao hatari, na hasa kwa mwanamke, lakini mwenyewe anasema amelishwa ujasiri na mafunzo ya kutosha kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo nchini (SIDO) mkoani Dodoma.
“Mwaka huu nimerina asali lita 88 kutokana na mizinga yangu 15. Ninategemea kwamba mwakani nitaongeza mizinga zaidi na hivyo mavuno ya asali yatakuwa makubwa. Nawashukuru sana SIDO kutokana na kutupatia mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki,” anasema.
Ellen ambaye ameolewa na kujaaliwa watoto watatu, anasema kwamba asingeweza kufikia hatua hiyo kubwa kama si jitihada za Ofisa Ugani wa Kata ya Ilindi, Anthony Sahali, ambaye aliwahamasisha wananchi wa kijiji cha Ilindi kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Anaongeza kwamba, ushawishi wake ulipokelewa kwa mtazamo tofauti kijijini hapo, lakini mwaka 2009 yeye na wenzake 43 wakaamua kuunda kikundi walichokipa jina la ‘Kilimo Nyuki’ wakiwa na lengo kujaribu kuona kama kweli wangefanikiwa.
“Kilichotupa nguvu zaidi na kutuhamasisha ni kuona viongozi wa serikali nao wakijiunga na kikundi hiki. Mwanzoni tulihisi ni utapeli, lakini kujiunga kwa viongozi hao kulitupa imani kwamba kumbe tunaweza kusonga mbele,” anaongeza na kusema kwamba mumewe, Sangula ambaye ni Diwani wa Kata ya Ilindi, alimpa moyo na kumtaka aendelee na harakati zake.
Ellen, ambaye ni Katibu wa kikundi hicho, anasema hata hivyo kwamba, Ofisa Ugani Anthony Sahali ambaye naye ni mwanakikundi, ndiye aliyewapa mwongozo wa namna ya kuanzisha kikundi hicho na kusaidia kupeleka maombi SIDO Mkoa wa Dodoma ili waweze kupatiwa mafunzo na hatimaye mkopo.
Anasema walipatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki mjini Dodoma mwaka 2009 na mkopo wa kwamba waliupata Januari 2010 ambapo kila mwanakikundi alipatiwa TShs. 200,000 zilizowawezesha kununulia mizinga ya kisasa yenye thamani ya TShs. 50,000 kila mmoja na nyingine kufungulia miradi midogo.
Kila mwanakikundi alipaswa kuchangia TShs. 25,000 na kiasi kingine kililipwa na SIDO wenyewe katika jitihada na kuwawezesha kupiga hatua kimaendeleo.
“Tulikubaliana kwamba kila mwanachama awe anachangia kiasi cha fedha kwenye kikundi au kiasi cha asali atakayovuna ambayo itauzwa na fedha kuingia kwenye mfuko wa kikundi. Tunashukuru kwamba mkopo wa kwanza tuliumaliza bila matatizo na mwaka huu tumepata mkopo wa TShs. 400,000 kila mmoja ambao tutaanza kuurejesha mwezi Novemba,” anasema.
Hata hivyo, Ellen anasema kwamba kikundi chao kimebaki na wanachama 27 baada ya wenzao 16 kujitoa mara baada ya kumaliza mkopo wa kwanza kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuyumba kwa biashara zao wakati wa msimu wa masika.
Lakini nyuki hawajamsaidia Ellen peke yake, kwani Medani Ibiga (37) ambaye ni mhasibu wa kikundi hiki, anasema kwamba ameweza kujenga nyumba, kununua ng’ombe karibu 20 na kuoa kutokana na ufugaji huo wa nyuki.
“Nimeanza kufuga nyuki kienyeji tangu nikiwa na miaka 18 nikitumia mizinga ya asili, lakini ukosefu wa elimu bora ulifanya nisione matunda yake. SIDO walipotoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki imenifumbua macho na sasa pato limeongezeka mara tatu,” anasema Ibiga.
Ibiga mwenye watoto wane anasema kwamba anamiliki mizinga 160 ya asili na 15 ya kisasa aliyonunua SIDO baada ya mafunzo, na kuongeza kwamba, kwa msimu huu tu amevuna lita 281 za asali pamoja na nta ya kutosha.
“Tatizo kubwa ni soko la uhakika la asali ndilo halipo au hatujalifahamu, lakini kwa kweli SIDO wametuokoa na mwaka 2010 walitusaidia baada ya kutukaribisha kwenye maonyesho yao ambako tuliweza kuuza bidhaa zetu,” anasema Ibiga.
Kwa upande wake, Rose Sudayi (36), anasema kwamba ufugaji huo wa nyuki umemsaidia kuendesha biashara yake ya kuku wa kienyeji pamoja na pombe inayotengenezwa kwa asali, hivyo kuokoa mazao yake ya nafaka ambayo sasa anayatumia kwa chakula tu yeye na familia yake.
“Huku vijijini tunapika sana pombe za kienyeji kwa kutumia nafaka, lakini tangu nijiingize kwenye ufugaji wa nyuki nimeachana na upikaji wa pombe za nafaka na kutengeneza kangara inayotumia asali. Fedha ninazozipata pia nazitumia kununulia nafaka pamoja na kuendeleza mradi wangu wa kuku,” anasema.
Anthony Sahali, Ofisa Ugani ambaye amekuwepo kwenye Kata ya Ilindi kwa miaka mitano sasa, anasema haikuwa kazi rahisi kuwashawishi wananchi kujiunga katika vikundi, lakini anashukuru kwamba mpaka sasa kikundi cha Kilimo Nyuki ni miongoni mwa vikundi vitatu vya Kata hiyo vilivyopata usajili katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
“Haikuwa kazi rahisi kuwashawishi wananchi kwani walikuwa wanaogopa kutapeliwa na kupoteza muda wao, lakini nashukuru hadi hapa tulipofikia. Kwa sasa Kata ina vikundi vitatu vilivyosajiliwa, vikiwemo vya Usuluza wa Mwino na Nyamuumi,” anasema Sahali.
Naye Lucas Sangula, Diwani wa Kata ya Ilindi, anasema anashukuru kuona miongoni mwa ahadi zake kwa wananchi za kuwaletea maendeleo zimeanza kutimia, kwani kuanzishwa kwa vikundi hivyo ni jitihada zake na Ofisa Ugani katika kuwahamasisha wananchi hao.
Anasema, hata hivyo, kwamba anawashukuru SIDO kwa kuwaunga mkono wananchi wa kata yake na akaomba taasisi nyingine za kijamii kuwasaidia wananchi wa vijijini kwani wanakopesheka na kwamba serikali za vijiji na kata ziko tayari kushirikiana kwa hali na mali na taasisi hizo.
Akizungumzia maendeleo ya vikundi vya Kata ya Ilindi, Meneja wa SIDO Mkoa wa Dodoma, Ismail Tego, alisema kwamba wananchi wa maeneo hayo ni waaminifu na wanaonyesha dhahiri kwamba wanapenda kujiletea maendeleo.
Tego anasema mpaka sasa shirika lake limetoa zaidi ya TShs. 70 milioni kwa vikundi mbalimbali wilayani Bahi, vikiwemo vya Kata ya Ilindi vinavyojishughulisha na ufugaji wa nyuki, kuku pamoja na uuzaji wa chumvi.
“Tutaendelea kushirikiana na wananchi wa vijijini kadiri itakavyowezekana, kwani lengo letu ni kuwakomboa wananchi hasa wa vijijini ambao wanaonekana kusahaulika na taasisi nyingine,” anasema.
Meneja huyo wa mkoa anasema, malengo yao ni kuwapatia elimu ya ujasiriamali pamoja na kuwahimiza waanzishe viwanda vidogo vya kusindika mazao yao ili waweze kupata faida zaidi.

Medani Ibiga, mhasibu wa kikundi cha Kilimo Nyuki akirekebisha mzinga. Wanaomtazama ni mwenyekiti wake Ellen Sangula na mwanakikundi Rose Sudayi

Mizinga ya nyuki ya kisasa iliyotolewa na SIDO - Dodoma

Ellen akilisha kuku wake wa kienyeji

Ofisa Ugani wa Kata ya Ilindi, Anthony Sahali, ambaye ameleta mabadiliko ya ujasiriamali kwa kuunda vikundi

Meneja wa Sido wa Mkoa wa Dodoma, Ismail M. Tego.

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. January 23, 2013 at 9:15 am

    mm mkazi wa moshi nimevutiwa na kikundi hicho nataka kujiunga nitawapataje

  2. April 7, 2014 at 12:18 pm

    NIMEPENDEZEWA NA HII BIZ NAOMBA NIFAHAMISHENI JINSI YA KUPATA MIZINGA YA KISASA NA ENEO LA KUJENGA MABANDA YA KUFUGIA

  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: