Home > All Stories > Walimu Mbarali watembea kilometa 52 kutwa

Walimu Mbarali watembea kilometa 52 kutwa

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kapunga Williard Sengele

Na Daniel Mbega, Mbarali

 

KWA Williard Sengele (54), mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kapunga wilayani Mbarali, mkoa wa Mbeya, siku huanza saa 10:00 alfajiri.

Huo ndio wakati anapoamka na kujiandaa kwa safari ya saa mbili kwa kutumia baiskeli kwenda shule, ambayo iko umbali wa kilometa 26 kutoka nyumbani kwake mjini Chimala.

Akiwa ndiye Mkuu wa Shule, anapaswa kuwasili shuleni saa moja asubuhi kabla ya walimu wengine na kabla ya masomo yanayoanza saa mbili asubuhi.

“Walimu wengi huchelewa kwa sababu wanaishi Chimala, ambako walihamia baada ya kufukuzwa mwaka 2006 kutoka kwenye nyumba walizokuwa wakiishi wakati NAFCO ikimiliki shamba la mpunga la Kapunga,” anasema Sengele.

Walimu wote walifukuzwa na mwekezaji, Export Trading Company iliyonunua shamba hilo lililokuwa linamilikiwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO).

Nyumba zote walizokuwa wakiishi walimu zilijengwa na NAFCO mwaka 1991 ambayo iliishawishi halmashauri ya kijiji kuihamisha shule kutoka kijijini Kapunga hadi kwenye eneo la shirika kama nia ya kuwapatia makazi bora walimu ambao walikuwa wakiishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa nyasi kijijini.

“NAFCO iliona bora kuhamishia shule kwenye eneo lao ambako kulikuwa na nyumba za ziada ambazo zingewatosha walimu waliokuwa na matatizo ya makazi wakati huo, lakini shamba lilipouzwa kila kitu kikakabidhiwa kwa mwekezaji, zikiwemo nyumba za walimu,” anasema Sengele.

Kwa sababu hiyo anasema tangu Januari 2007, walimu wamekuwa wakitembea ama kuendesha baiskeli kilometa 52 kila siku kwenda na kurudi shule, hali inayoathiri taaluma kwa kuwa wengi huchelewa shule, hivyo kukosa vipindi.

Sengele anasema kufuatia kufukuzwa kwao, kwa mwezi mmoja tangu Desemba 6, 2006 hadi Januari 6, 2007 yeye na familia yake ya watu sita alilazimika kuishi darasani.

“Shule ilikuwa imefungwa kwa likizo ya Desemba. Nilitumia ofisi yangu kama chumba cha kulala mimi na mke wangu na watoto wangu wanne walilala kwenye ofisi ya walimu,” anasema.

Lakini Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) unatambua kwamba kuwapatia nyumba walimu wanaoajiriwa na kupelekwa maeneo ya vijijini na yasiyofikika, ni moja ya motisha kwao.

Shule hiyo ina walimu 9 tu, ikiwa ni nusu ya walimu wanaotakiwa. Hali hii inafanya mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 80, kinyume na utaratibu ambao kwa wastani wa taifa, mwalimu mmoja anapaswa kufundisha wanafunzi 45.

Shule ya Msingi Kapunga ilisajiliwa rasmi mwaka 1977 ikiwa na hati Na. MB 08/1/022, ilihamishiwa kwenye eneo la NAFCO mwaka 1992 kutoka kijijini Kapunga.

Kwa sasa shule ina wanafunzi 624 walio katika mikondo 16, lakini idadi ya walimu inazidi kupungua pamoja na mahudhurio.

Wastani wa sasa wa mahudhurio ni asilimia 75, na kwa mujibu wa Sengele, kiwango hicho kinasababishwa na umbali kutoka shule kwa walimu na wanafunzi.

Kwa hali hii anasema hata kiwango cha ufaulu kimekuwa kikishuka kila mwaka: “Nilipokuja mwaka 2003 ni wanafunzi nane tu kati ya 22 waliofaulu kuingia sekondari mwaka huo, lakini idadi ikaongezeka mwaka 2004 na watoto 13 kati ya 16 walikwenda sekondari.

“Mwaka 2005, wanafunzi 20 kati ya 35 walijiunga na kidato cha kwanza.”

Aidha, takwimu za shule hiyo zinaonyesha kwamba mwaka 2006, watoto 34 kati ya 61 walijiunga na kidato cha kwanza; mwaka 2007, watoto 30 kati ya 36 walifaulu. Lakini mwaka 2008 waliochaguliwa walikuwa 30 kati ya 63 na mwaka 2009 wakashuka hadi 20 kati ya 57; mwaka 2010 waliochaguliwa walikuwa 23 kati ya 60.

“Hatujui kitakachotokea mwaka huu kwa sababu hata walimu wamepoteza morali,” anaongeza kusema.

Kwa mwalimu Donata Chaula ambaye hiyo ndiyo ajira yake ya kwanza, anasema kwa miaka mitatu amekuwa akitumia Sh 4,000 kila siku akilipia usafiri wa pikipiki kwenda na kurudi shule.

“Sehemu kubwa ya mshahara wetu inaishia barabarani tunapokuja shule. Kwa mwezi natumia Sh 80,000 kwa usafiri tu,” anasema.

Abbas Mwamuli anayesoma darasa la sita shuleni hapo anaishi kijiji cha Mwashikamili, ambacho kipo umbali wa kilometa 10 kutoka Kapunga. Yeye anasema analazimika kuamka saa 11:00 alfajiri na kuendesha baiskeli kwa saa moja na nusu kwenda shule.

“Ni mateso makubwa kwetu sisi tunaoishi mbali kutoka shuleni. Pengine Serikali ingeweza kutusaidia kwa kujenga shule katika kila kijiji ili kutunusuru tusihatarishe maisha kila siku,” anasema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kapunga, Ramadhan Nyoni, anasema wanakijiji walijenga nyumba moja ya walimu mwaka 2010 katika eneo ambalo awali shule hiyo ilikuwa imejengwa. Serikali ikawasaidia mabati ya kuezekea na mbao, lakini wameshindwa kumalizia jengo la pili kutokana na misukosuko ya mwekezaji.

“Tulitaka kutatua tatizo la nyumba kwa walimu wetu na kufikiria kujenga sekondari, kwani hatuna hata sekondari moja (kwenye Kata ya Itamboleo). Lakini kutokana na matatizo haya hatujui tuwasaidieje walimu na watoto wetu,” anasema.

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji, mwekezaji anapaswa kuendeleza huduma za jamii kama shule na zahanati katika maeneo yanayozunguka mradi wake.

Sergei Bekker, Meneja uzalishaji wa Kapunga Rice Project Limited, kampuni ya ubia inayosimamia mradi huo, anasema dhamira yao ni kujenga shule katika kijiji cha Site One na kuihamisha mahali ilipo sasa ili kuisaidia jamii.

“Hatuwezi kujenga shule kwenye kijiji cha Kapunga kwa sababu ni ardhi yetu. Tulitaka kujenga kule Matebete, lakini Serikali imesema wananchi wale wanapaswa kuhamishwa, kwani ni eneo la TANAPA. Wakazi wa Kapunga hawataki kututambua kama wawekezaji na hili ndilo tatizo linalochelewesha mradi wa ujenzi wa shule,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Mbarali Wilson Mabuba, anasema anafahamu matatizo katika shule ya msingi Kapunga, lakini akagoma kuelezea zaidi kwa maelezo kwamba si msemaji wa halmashauri.

“Natambua kwamba walimu wa Kapunga wanateseka, na kama unavyojua, ufaulu unashuka kila mwaka. Bahati mbaya mimi si msemaji, mtafute Mkurugenzi wa Halmashauri anaweza kueleza zaidi,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, George Kagomba, anasema mgogoro wa Kapunga ni wa kisheria na unaweza kutatuliwa na Serikali Kuu, siyo halmashauri yake.

“Ninayafahamu matatizo hayo, lakini mkataba ule ulikuwa kati ya mwekezaji na Serikali na walikubaliana kwamba kama tatizo lolote litatokea wanaweza kulimaliza Mahakama Kuu, kwa hiyo acha Serikali kuu ilimalize kisheria na kiufundi,” anasema.

Alipotafutwa ili kutoa maelezo zaidi, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, alisema tatizo la walimu wa Kapunga lilikuwa bado kwenye ngazi ya halmashauri ya wilaya na hakuwa na taarifa zozote.

“Nenda kamuulize Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, naamini wanaweza kulitatua, na kwa upande wangu, sina taarifa zozote kuhusu eneo hilo,” alieleza.

 

 

 

 

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: