Home > All Stories > Ugonjwa hatari usiotibika,wahofiwa kuingia nchini

Ugonjwa hatari usiotibika,wahofiwa kuingia nchini

Leon Bahati
INGAWA Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inasema haujaripotiwa sehemu yoyote nchini, ripoti za kimataifa zinaonyesha kuwa tayari umeingia.

Ni ugonjwa unaoathiri ubongo na kusababisha mtu kusinzia hovyo na hata kumfanya ashindwe kufanya kazi na kula.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ugonjwa huu ambao bado haujafahamika vyema kwa wanasayansi, unawapata zaidi watoto wa umri kati ya miaka mitano na 15.

Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa afya ugonjwa huo humlemaza mtoto kiasi cha kushindwa kucheza na wenzake, kuhudhuria vipindi darasani na kula. Hali hiyo humfanya akonde kula na hatimaye kufa.

Tayari mamia ya watoto Kaskazini mwa Uganda na Sudani ya Kusini wameugua na wengi wao wamekufa.

Ni ugonjwa wa namna gani?
Kwa namna ugonjwa huu unavyoanza siyo rahisi mtu kuufahamu haraka kwa sababu tu unaweza kuona mtoto akiwa na dalili za uchomvu na pengine waweza kudhani ni magonjwa ya kawaida.

Mmoja wa waliotumia muda mwingi kuchunguza ugonjwa huo ni Mtaalamu na Mtafiti wa maradhi ya Ubongo, Profesa Peter Spencer, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Afya cha Kimataifa (HSU).

Profesa Spencer anasema huu ni ugonjwa  mgeni hapa duniani na umepewa jina la kusinzia au kwa namna nyingine kutikisa kichwa kunakoandamana na kuinamisha kichwa mbele.

Kulingana na uchunguzi wa kitaalamu, anasema ugonjwa huo ulianzia kwenye moja ya maeneo nchini Sudani Kusini kwenye miaka 1960.

Mwenye ugonjwa huo anaonekana kuwa na   uchovu kupita kiasi, uwezo wa akili hupungua na huonekana kama mlemavu kutakana na viungo vyake kulegea na wakati mwingi kuonekana mwenye usingizi.

Profesa Spencer anasema tayari ugonjwa huo umesambaa katika nchi mbili za Afrika Mashariki; Uganda na Tanzania.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba ugonjwa huo unaweza kupatikana katika nchi tatu tu duniani na wanafanya mikakati ya kuangalia jinsi ya kuudhibiti usienee sehemu nyingine.

Dalili za ugonjwa huu zinaelezewa kuwa siyo za kawaida na wakati mwingine zinachanganya.

Moja ya dalili hizo, anasema ni kusinzia, kutikisa kichwa kwa kuinamia mbele, kukakamaa na wakati mwingine huanguka hovyo mithili ya mtu mwenye kifafa.

Wataalamu wanasema hali hiyo inatokana na athari kwenye ubongo ambapo inaonekana utendaji kazi unapungua siku hadi siku.

Profesa Spencer anasema hali hiyo inaelezewa kuwa humuathiri mtoto kwa njia nyingi zikiwepo za kushindwa kula vizuri, viungo kutofanya kazi ipasavyo na mara nyingi huandamana na maradhi ya utapiamlo.

Maradhi hayo ya ubongo, anayaelezea kuwa huandamana pia na athari za moyo jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya watoto.

Anasema kutakana na mazingira hao, mtoto hukataa kula, hudhoofika na baadae hufa.

Tiba yake
Hadi hivi sasa Profesa Spencer anasema hakuna tiba wala chanjo ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Tatizo kubwa anasema bado wataalamu hawajabaini chanzo cha ugonjwa huo japokuwa uchunguzi unaonyesha kuwa hakuna maambukizi ya moja kwa moja kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu mwingine.

Hata hivyo anasema hueda katika suki zijazo kipimo cha scanner kikatumika katika kubaini watoto wenye maradhi hayo.

Pamoja na kutokuwepo kwa tiba, Profesa Spencer  anasema wanapendekeza baadhi ya dawa zilizopo kwenye mfumo wa tiba kutumika ili kumsaidia mgonjwa kukabiliana na athari za ugonjwa huo.

Miongoni mwa dawa hizo ni  sodium valproate na phenobarbitol. Vile vile dawa za kutibu malaria zinatumika kama moja ya mbinu za kupunguza makali ya ugonjwa.

“Huu ni ugonjwa ambao unadhoofisha mwili na akili pia,” alisema Profesa Spencer akibainisha kuwa mtoto anaweza akaishi nao kwa miaka mitatu au zaidi, lakini hatima yake ikawa ni kifo.

Anasema ni watoto wachache ambao wameweza kupona ugonjwa huu; “wengi wao hufa.”

Anasema hakuna maelezo ya kitaalamu ambayo yanaonyesha chanzo cha ugonjwa huu lakini anafikiri kuna uwezekano mkubwa ukawa unasababishwa na aina fulani ya minyoo ambayo kitaalamu inajulikana kwa jina la Onchocerca volvulus.

Aina hiyo ya minyoo anaielezea kuwa kuna uwezekano wakawa wanasambazwa na aina fulani ya vipepeo weusi.

Vipepeo hao pia anasema wanasababisha magonjwa ya upofu na ndio maana sehemu ambazo ugonjwa huo umekomaa watoto kadhaa wanapata tatizo la kuona.

Mtafiti mwingine wa ugonjwa huo ambaye aliufanyia uchunguzi ugonjwa huo akiwa Tanzania, Andrea Winkler anasema minyoo hao wanapokuwa kwenye mwili wa binadamu hueda hadi kwenye ubongo na kusababisha madhara hayo.

Winkler anasema anaamini kuwa athari za kuwapo aina hiyo ya minyoo indiko kunakosababisha mazingira ya kuzalisha kemikali ama ukosefu wa aina fulani ya vitamini, ambazo athari zake zinakuwa ni kwenye ubongo.

Mojawapo ya aina ya vitamin ambayo inahisiwa kuwa ukosefu wake husababisha ugonjwa huo ni  B6  ambayo kwa jina la kitaalamu hujulikana kama pyridoxine.

Maeneo yaliyoathirika
Maeneo yaliyoathirika yanaelezewa kuwa ni  White Nile na maeneo karibu na Juba ambao ni mji mkuu wa Sudani Kusini na eneo la kusini mwa nchi hiyo ambalo linapakana na Uganda.

Uganda imeathirika zaidi katika eneo lake la Kaskazini ambalo kwa miaka kadhaa lilikumbwa na vita kati ya Serikali na waasi wa kikundi cha Lord Resistance Army (LRA).

Kwa mujibu wa wataalamu hao, eneo la Kusini mwa Tanzania liliwahi kuripotiwa kuwapo kwa mtoto aliyekuwa na dalili za ugonjwa huo miaka ya 1962.

Lakini katika miaka ya karibuni eneo la Sudani Kusini na Kaskazini mwa Uganda, ugonjwa huo unaathiri mamia ya watoto na tayari vifo kadhaa vimeripotiwa kutokea.

Kumbukumbu za mwaka 2009 zinaonyesha Uganda ilikuwa na wagonjwa zaidi ya 2000.

Katika kipindi cha mwaka huu, wataalamu hao wanasema wanaamini ugonjwa huo pia upo Tanzania.

Tamko la Tanzania
Kaimu Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Petro Ramadhan anasema ingawa kumekuwepo na maelezo hayo, wao hawajapata taarifa kamili inayothibitisha kuwapo kwa ugonjwa huo nchini.

“Kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa ya kuambukiza unaofanyika kila siku nchini, hakuna mkoa au wilaya iliyotoa taarifa kwa wizara kuhusu kuwepo kwa mgonjwa yeyote mwenye dalili za ugonjwa huo,” alisema Ramadhan.

Lakini akaonya kuwa taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo kwa nchi jirani ya Uganda, ni rahisi ukapatikana nchini.

Kwa sababu hiyo anasema tayari wamesambaza taarifa kwa wataalamu wote wa afya wa mikoa na wilaya nchini kufuatilia kwa makini na kutoa taarifa pale atakapopatikana mgonjwa mwenye dalili hizo.

Isitoshe anasema wananchi nao wanapaswa kuwa macho na kubaini iwapo mgonjwa wao atakuwa na dalili hizo ili ziripotiwe na hatua za kukabiliana na ugonjwa huo zichukuliwe.

SOURCE: Mwananchi

http://www.mwananchi.co.tz/habari/3-habari-za-mikoani/21179-ugonjwa-hatari-usiotibikawahofiwa-kuingia-nchini

 

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: