Home > All Stories > DCI arudishiwa jalada la madai ya kulishwa sumu Dk Mwakyembe

DCI arudishiwa jalada la madai ya kulishwa sumu Dk Mwakyembe

MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, amelirudisha kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), jalada la kesi ya waliodai ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi,  Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi, DPP Feleshi alisema , baada ya kulipitia jalada hilo, ameona alirudishe tena polisi ili likafanyiwe kazi zaidi.
Ofisi ya DCI ilikuwa imelipeleka jalada hilo kwa DPP ili atoe baraka za kupeleka kesi hiyo mahakamani.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alipotakiwa kueleza hatua ambazo ofisi yake inachukua baada ya kurejeshwa kwa jalada hilo alisema “Mimi sina usemi (na kukata simu).”
Manumba alilipeleka jalada hilo kwa DPP baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, mwezi uliopita akisisitiza atawapeleka mahakamani wote waliotoa taarifa kuwa ugonjwa uliokuwa unamsumbua Dk Mwakyembe unatokana na kulishwa sumu.
Manumba alisema , uchunguzi uliofanywa na polisi pamoja na kupata taarifa kutoka hospitali ya Appolo nchini India, ambako Dk Mwakyembe alikuwa akipatiwa matibabu, zinaonyesha kuwa ugonjwa wake hautokani na kulishwa sumu.
Wakati DCI alipopeleka faili hilo kwa DPP, Dk Mwakyembe alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema: “Napata tabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa ‘nyingine’ na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au ‘walisomewa!’
“Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo.
Mkakati huo wa DCI ulizua malumbano na misimamo iliyoashiria kuwapo kwa kauli zinazokinzana na kuzihusisha wizara nne tofauti iwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mambo ya Ndani ya Nchi, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ujenzi.
Kuna wakati Waziri Sitta alinukuliwa akisisitiza kwamba hisia zinaonyesha ugonjwa huo unatokana na kulishwa sumu wakati Wizara ya Afya ilionyesha kushangaa ripoti hiyo huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsa Vuai Nahodha akisema kuwa hajui zilikopatikana taarifa hizo na kuamua kuunda tume ya kuchunguza kwa undani kuhusu suala hilo.
Hata hivyo baada ya kurejea nchini Ijumaa iliyopita akitoa India alikoenda kwa matibabu, Dk Mwakyembe alisema, kwa sasa amepona kabisa na anaendelea na kazi za kulijenga taifa pasipo na wasiwasi wowote.
Alizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, alisema ugonjwa uliokuwa ukimsumbua unafahamika kitaalamu kwa jina la Popular Scleroderma.
Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo yaliifanya Serikali kuamua kumpeleka Hospitali ya Appolo, Oktoba 9 mwaka jana na kurejea Desemba.
Dk Mwakyembe alisema anachoshukuru hadi sasa ni kwamba afya yake imeimarika kutokana na shinikizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza Serikali kumpa kipaumbele wakati wote akiwa nchini na India hatua ambayo imemwezesha kufika hapo alipo.

Mtaalamu auzungumzia
Mtaalamu wa afya ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema ugonjwa huo wa ‘Popular Scleroderma’ unasababishwa na chembechembe hai nyeupe kushambulia kitu kigeni kilichoingia kwenye mwili na kusababisha magonjwa ya ngozi.
Alisema chembechembe hizo zinaweza kusababisha ngozi ya mwili kuharibika… “Ni magonjwa yanayosababishwa na chembechembe hai nyeupe kujikataa zenyewe na kusababisha ugonjwa wa ngozi na mifupa.”

CHANZO: MWANANCHI

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: