Home > All Stories > Serikali yamjibu Lowassa

Serikali yamjibu Lowassa

SERIKALI imetoa takwimu za ajira kwa vijana nchini ikiwa ni majibu kwa kauli za mara kwa mara za Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye amekuwa akisema tatizo hilo ni kubwa akililinganisha na bomu linalosubiri kulipuka.
Lowassa amenukuliwa katika matukio manne tofauti kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu, akionya tatizo hilo la ajira kwa vijana kwamba linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Jana, Waziri wa Kazi na Ajira alisema tatizo hilo haliwezi kufafanishwa na bomu na kusema wanaosambaza uvumi huo hawaitendei haki Serikali, kwani tatizo hilo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 hadi asilimia 11.7, mwaka 2006.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kabaka alitoa ufafanuzi wa hali ya ajira nchini na hatua ambazo Serikali inachukua kushughulikia tatizo hilo.
“Hali halisi ya ukuaji wa uchumi nchini ni nzuri lakini, haiwezi kuonekana kama wananchi wake ni maskini na hawana ajira. Hata hivyo, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali kushughulikia suala hilo ikiwamo la kuhimiza uwekezaji nchini,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli na kudai Serikali hayaijafanya kitu wanakuwa hawaitendei haki.”
Alisema utafiti uliofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa tatizo hilo limepungua kwa asilimia 1.2.

Mikakati
Waziri Kabaka alisema utafiti uliofanywa na NBS mwaka 2006 ikishirikiana na wizara hiyo unabainisha kuwa nguvu kazi ya Tanzania ni 20.6milioni kati ya watu 37.5 milioni, kwa wakati huo.
Alisema kutokana na utafiti huo, watu 18.3milioni sawa na asilimia 88.3 ya watu hao 20.6milioni walikuwa na ajira huku waliokuwa kwenye ajira ya sekta rasmi wakiwa ni 17milioni sawa na asilimia 92.7.
Kabaka alisema katika utafiti huo, watu 1.3milioni walikuwa kwenye ajira isiyo rasmi huku utafiti ukibaini kuwa kila mwaka watu 800,000 hadi milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira.
“Utafiti unaonyesha hali ya ukosefu wa ajira nchini umeshuka kidogo kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 na kufikia asilimia 11.7 mwaka 2006, hata hivyo kiwango hicho ni cha juu kwa nchi kama Tanzania ambayo haina huduma za kinga kwa watu wasio na ajira,” alisema Kabaka.
Waziri Kabaka alisema pamoja na kushuka kwa kiwango cha ajira, bado kiwango cha ukosefu wa ajira ni kikubwa huku kikitofatutiana baina ya kundi moja na jingine akisema Tanzania siyo kisiwa hivyo, tatizo linaloikumba dunia la ukosefu wa ajira pia linaikumba nchi hiyo.
Alitaja mikakati ya Serikali kuwa ni pamoja na utekelezaji wa mipango mbalimbali yenye lengo la kukuza ajira ambayo ni pamoja na mpango wa mafunzo yenye kuwezesha vijana kujiajiri, mfuko wa maendeleo ya vijana, mpango wa kukuza ajira kwa vijana na mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kukuza ajira.
Kabaka alitaja mipango mingine kuwa ni ule wa uwekezaji katika elimu na mafunzo, kujengea uwezo mamlaka za Serikali za mitaa (LGAs) na ajira za moja kwa moja zinazotolewa na Serikali kupitia sekta mbalimbali.
“Serikali imetoa ajira kwa walimu 15,000 wa shule za sekondari na msingi na pia kwa kipindi cha miaka mitano 2007 hadi 2011, ajira 414,679 zimepatikana kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC),” alisema Kabaka.
Waziri Kabaka alibainisha mpango kabambe uliowekwa na Serikali katika kukabiliana na tatizo la ajira, ambao alisema hadi kufikia mwaka 2015, itakuwa imepunguza tatizo la ajira kutoka asimilia 11.6 ya mwaka 2006 hadi kufikia asilimia tano.
Alisema katika kutekeleza hilo, Serikali imeanza kuchukua hatua na kwamba imeanda programu ya kwanza itakayolenga kutambua vijana wote wenye taaluma aina ya ujuzi walionao katika kila wilaya hapa nchini.
“Programu hii ambayo utekelezaji wake unatarajia kuanza mwaka wa fedha wa 2012/13, imejikita katika kuwatambua vijana na shughuli zao ili kuwajengea uwezo katika kukuza tabia ya kijasiriamali, kuwawezesha kupata ujuzi wa kujiajiri na kukuza soko la bidhaa za ndani kwa kuweka mazingira kutumia bidhaa za Tanzania,” alisema Kabaka.
Alisema pia mpango huo umejikita kuwezesha kijana mmojamoja au kikundi kujiajiri, vijana wasomi na wenye ujuzi wanaohitimu katika vyuo vya elimu ya juu kujiajiri na kutengeneza mazingira ya kuajiri wengine na pia kuwezesha sekta binafsi na taasisi za umma kuwekeza katika sekta zenye kipaumbele katika kutoa ajira.
Waziri Kabaka alisema Serikali imejipanga kutekeleza mpango wa kukuza ajira katika maeneo ya mikoa na wilaya ili kuwezesha kupunguza tatizo la ajira na kuwafanya vijana wasikimbilie mijini.

Maana ya ajira
Akinuuku tafsiri inayotumika duniani na kutambuliwa na Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO), Waziri Kabaka alisema maana ya ajira ni shughuli yoyote halali anayoifanya mtu mwenye umri wa kufanya kazi kwa kujipatia kipato na kwa kawaida shughuli hiyo ni ya hiari inayotambuliwa kisheria na hufanywa kwa saa 40 hadi 45 kwa wiki.
Alisema ukosefu wa ajira ni hali ambayo hutokea wakati watu walioko kwenye umri wa kufanya kazi na ambao wangependa kufanya kazi wanatafuta bila ya kuipata.
“Tafisiri hii ya kimataifa haiwajumuishi wale wasiotafuta kazi, wasiopenda kufanya kazi hata kama hawana kazi,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Lakini tafisiri inayotumika zaidi Tanzania inatambua wote wasio na kazi na ambao wako tayari kufanya kazi bila kujali wanatafuta kazi au la na inawahusisha hata wasio na uhakika wa kufanya kazi hata ya siku moja.”
Alitaja aina tatu za ajira ambazo ni kazi ya staha, kazi chini ya kiwango na ajira maskini.
Alisema ajira za staha ni zile ambazo zina tija kiusalama, heshima haki za wafanyakazi na kipato cha kutosha, wakati ya ile ya chini ya kiwango ni ile ambayo haitoshelezi kutumia uwezo, muda na taaluma yote ambayo ambayo mhusika anayo. Ajira maskini ni ile ambayo kipato kinachopatikana ni cha chini ya kiwango kisichomwezesha mtu kuishi.
Akirejea utafiti wa ILO wa mwaka 2010/11, Waziri Kabaka alisema ripoti hiyo inaonyesha hali ya umaskini na ukosefu wa ajira duniani ni kubwa. Watu 205 milioni dunia kote mwaka 2010 hawakuwa na ajira.
Alisema idadi hiyo ilikuwa sawa na ongezeko la nguvu kazi isiyo na ajira duniani ya watu 27.7 milioni kulinganisha na ile ya mwaka 2007.
Alisema sababu za ongezeko la ukosefu wa ajira kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni kutokana na utandawazi, maendeleo ya mawasiliano, mabadiliko ya teknolojia ambayo hayahitaji nguvu kazi nyingi katika utendaji kazi na kudidimia kwa nguvu za kiuchumi hasa katika nchi zinazoendelea.

Lowassa na ajira
Novemba 15, mwaka jana akiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Makasa, Parokia ya Nyakato, Mwanza, Lowassa alionya kuhusu tatizo hilo na kulitaka lisaidie kujenga vyuo vya ufundi.
Alitoa takwimu akisema utafiti wa mwaka 2006, ambao hata hivyo, hakusema ulifanywa na taasisi gani, ulionyesha tatizo hilo kwa sasa limekuwa na kufikia asilimia 15 huku likigusa zaidi vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 ambao ndiyo nguvukazi ya taifa… “Ninapozungumza hili siyo nia yangu kumlenga mtu. Mimi ni Yohana Mbatizaji, hii ni sauti inayolia nyikani.”
Novemba 29, mwaka huo wa jana akiwa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKT), Usharika wa Amani Sabasaba, Singida, Lowassa alirudia tena suala hilo la tatizo ajira.
Mapema mwaka jana, Lowassa pia alifanya mkutano na waandishi wa habari Mjini Arusha na kuzungumzia tatizo hilo la ajira ambalo alilifananisha na bomu.
Jumatatu iliyopita, Lowassa alirejea kauli hiyo alipokuwa katika sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara akisema: “Nawaomba maaskofu katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala la tatizo la ajira kwa vijana…. hili kama tulivyosema ni bomu linalosubiri kulipuka…”

CHANZO: MWANANCHI

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: