Home > All Stories > Ufisadi kuifikisha Mbomipa kortini

Ufisadi kuifikisha Mbomipa kortini

Na Mwandishi Wetu

VIJIJI nane kati ya 21 vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (Mbomipa) vimetishia kwenda mahakamani kupinga mikataba ya uwekezaji inayodaiwa kuwa mibovu.

Vijiji hivyo nane vinadai kwamba, mikataba hiyo imetandwa na mazingira ya ufisadi na kwamba haiko katika mazingira ya kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wenyeviti wa vijiji vinavyopinga mikataba hiyo, David Ndelwa, aliliambia Kwanza Jamii-Iringa kwamba, kampuni hizo zinakiuka mikataba huku akizituhumu kupewa upendeleo na baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo.

Ndelwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Tungamalenga, alisema vijiji hivyo nane vinavyounda jumuiya hiyo inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani Iringa, vimegoma kupokea gawiwo la kila mwaka linalotokana na mapato ya uwekezaji.

Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Tungamalenga, Mahuninga, Makifu, Mapogoro, Kitisi, Idodi, Mlowa na Mafurutu.

“Kwa kupitia mikataba waliyopewa, kampuni hizo zilipaswa kujenga hoteli za kitalii katika maeneo waliyopewa, lakini tangu waingie mikataba hiyo hakuna dalili za kujenga na badala yake zinaendesha shughuli za uwindaji na utalii wa picha katika maeneo hayo,” alisema.

Alisema mojawapo ya kampuni hizo iliomba kujenga hoteli ya kitalii, lakini badala yake imekuwa ikifanya uwindaji wa utalii.

“Kampuni nyingine inadaiwa kuzidisha idadi ya Simba na Pundamili waliopaswa kuwindwa, jambo ambalo linaonyesha kuzingirwa na ufisadi na tunahisi huenda hata viongozi wa juu serikalini wanahusika,” aliongeza.

Kwa mujibu wa taratibu za uwindaji wa kitalii, wakati kampuni hizo zinapokwenda kuwinda ni lazima awepo Ofisa Wanyamapori wa Wilaya (DGO), Skauti wa Kijiji (Village Game Scout) pamoja na ofisa wanyamapori wa serikali.

Ndelwa alisema jitihada zao kuzitaka kampuni hizo zitimize vifungu vyote vilivyopo kwenye mikataba hazijazaa matunda na kuifanya jumuiya hiyo ipoteze mapato mengi.

Alisema hatua hiyo imekifanya kijiji chake cha Tungamalenga na vijiji vingine saba vikatae kuchukua mgao wa fedha zinazotolewa kwa kila kijiji kila mwaka kama gawiwo kutokana na mapato yatokanayo na uwindaji.

“Mwaka 2009 kila kijiji kilipata Sh 500,000, mwaka 2010 Sh 2.5 milioni, lakini katika hali ya kushangaza mgao kwa mwaka jana ulikuwa Sh 800,000 ambazo tulikataa kuzipokea,” alisema.

Amehoji, kwa niaba ya wenzake, ni kwa vipi kiwango hicho cha gawiwo kishuke kwa zaidi ya theluthi mbili ya kile cha mwaka 2010, wakati ambapo walitegemea kuona kinapanda.

Alisema katika kuutatua mgogoro huo, wamekwishakaa vikao viwili, kati yake kimoja kilihudhuriwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Kapteni (mstaafu) Aseri Msangi.

Malalamiko mengine ya vijiji hivyo nane ni kuhusu mkanganyiko wa nani hasa mwekezaji katika eneo hilo baada ya viongozi wa Mbomipa kuingia mkataba na kampuni nyingine kabla ya mwekezaji wa kwanza kujamaliza mkataba wake.

Hoja nyingine ni ya kukiukwa kwa Katiba ya Mbomipa inayosema vijiji vinavyounda jumuiya hiyo ni vile vilivyo karibu na hifadhi na ambavyo vimetoa ardhi yao kwa ajili ya eneo hilo tengefu.

“Vijiji hivi nane, na vingine vinne ambavyo viko Pawaga, ndivyo hasa vinavyostahili kuwemo kwenye Mbomipa, lakini sasa kuna vijiji vingine tisa ambavyo havikutoa ardhi navyo vimeingizwa kinyemela,” alisema Ndelwa.

Alisema kwamba, hata viongozi wa sasa wa Mbimipa wanatoka katika kijiji cha Kinyika ambacho hakikutoa ardhi kwa mujibu wa katiba yao.

Viongozi hao, Mkumbata (Mwenyekiti), Nyamatana (Makamu Mwenyekiti) na Mkombilenga (Katibu), waliingia madarakani baada ya kuuengua uongozi wa awali unaodaiwa kuingia mikataba hiyo mibovu.

Leonard Chengula, mwenyekiti aliyeenguliwa, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia sakata hilo, hakuweza kupatikana.

Naye mwenyekiti wa sasa wa Mbomipa, Mkumbata, aliliambia Kwanza Jamii-Iringa kwamba, hakuna mgogoro wowote ndani ya jumuiya hiyo na kubainisha kuwa wamekwishaafikiana na wahusika ili wachukue hundi zao.

“Mbona tulikwishayamaliza na tumewaambia waje wachukue hundi zao?” alihoji mwenyekiti huyo na kusema kwamba badala ya Sh 800,000 waliongeza Sh 200,000 katika fungu hilo.

Hata hivyo, Kwanza Jamii-Iringa bado inafuatilia kwa kina suala hili.

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: