Home > All Stories > ‘Vurugu Zanzibar zina mkono wa vigogo’

‘Vurugu Zanzibar zina mkono wa vigogo’


KANISA la Pentekoste Tanzania limedai kuwa vurugu zilizotokea visiwani Zanzibar na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali, zina msukumo wa baadhi ya viongozi wa siasa na dini.

Kiongozi mkuu wa kanisa hilo, William Mwamalanga aliliambia Tanzania Daima jana kuwa, baadhi ya viongozi wa siasa wanaouchukia muungano, na wale wenye malengo ya kidini, waliwatumia vijana kufanya vurugu hizo.

“Kuna siri nzito iliyojificha katika vurugu hizo. Wapo baadhi ya viongozi nyuma ya vurugu hizo kwani muungano umetumiwa kama kigezo.

“Chokochoko za muungano hazijaanza leo wala jana, maana tunafahamu wazi kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiupinga muungano huo ndani ya Bunge na hata nje, hivyo imefika wakati kwa watawala wetu kuwa wakweli juu ya suala hilo,” alisema.

Mchungaji huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Kupambana na Dawa za Kulevya, alisema kuwa kauli za baadhi ya viongozi zinazotolewa juu ya suala hilo, zimekuwa chachu za vurugu hizo.

Alidai kuwa, anaamini matatizo ya muungano hayatamalizwa kwa kupatikana katiba mpya, bali kinachopaswa ni viongozi wanaofahamu umuhimu wa suala hilo kuweka wazi kwa wananchi ili waweze kuujua kwa undani.

“Watawala wawaeleze vijana umuhimu wa suala hilo hata kama kuna mchakato wa katiba mpya bado itakuwa shida, kwa kuwa vijana hawaelewi ulazima wa ushirikiano huo,” alifafanua.

Alisema watawala wanapaswa waandae kipindi maalum ili kuujadili muungano huo, maana kwa sasa suala hilo limevuka mipaka na kutumiwa kama kigezo cha uhalifu na uvunjifu wa amani.

Hata hivyo, alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema kupata muda na kukutana na wazee wa visiwa hivyo pamoja na viongozi wa kisiasa ili kutafuta suluhu ya kudumu juu ya suala hilo.

UTALII HAUJAVURUGWA

Katika hatua nyingine, serikali imesema vurugu zilizotokea Zanzibar hazikuathiri soko la utalii kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Kenya na katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema mitandao na vyombo hivyo havikusema ukweli na vina lengo la kuichafua Tanzania.

Alisema hali ya amani katika Mji Mkongwe imetulia na kwamba hakuna taarifa zozote za uharibifu wa maeneo ya vivutio vya utalii wala kuchomwa moto kwa hoteli yoyote ya kitalii.

“Serikali inawahakikishia wananchi na jumuiya ya kimataifa kuwa, hayo yalikuwa matukio ya kipekee na ya kupita, na hatua zimechukuliwa na Jeshi la Polisi kuongeza usalama kwa wakazi na watalii,” alisema Nyalandu.

Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa matukio ya kuporwa kwa watalii na vibaka ambapo hivi karibuni watalii wanne wamefanyiwa vitendo hivyo katika maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam ambavyo vimefanywa na watu waliotumia magari na pikipiki.

Hivi karibuni katika mji wa Zanzibar, kumetokea vurugu zilizosababisha kuchomwa kwa makanisa pamoja na shule jambo ambalo viongozi mbalimbali wa serikali na wa kidini wametoa tamko.

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: