Home > All Stories > Iringa yapoteza 70% ya Nyanya

Iringa yapoteza 70% ya Nyanya


• Zaharibika kutokana na ukosefu wa soko
• Walilia kujengwa viwanda vya usindikaji

Na Daniel Mbega

CHINI ya miti ya mikaratusi, kando ya Mto Mlowo, vijana wanaonekana wakijaza nyanya kwenye matenga ya mbao huku pembeni yao kukiwa na malundo makubwa ya zao hilo.
“Hii ni hasara kubwa, nimekuja na matenga hamsini, lakini inaonekana yametoka thelathini tu, haya malundo yote ni nyanya zilizolainika (masalo) ambazo haziwezi kwenda mahali popote,” anasema Jacob Kamota, mkulima wa nyanya kutoka Kijiji cha Iyayi, Kata ya Image wilayani Kilolo.
Jacob analalamika kwamba, huko shambani pia ameacha malundo ya nyanya zisizofaa kusafirishwa, ingawa zinafaa kwa matumizi ya nyumbani au hata kwa kusindikwa, hali ambayo inazidi kumtia umaskini badala ya kujikwamua kiuchumi.
“Sina mahali pa kuzipeleka, laiti kungekuwepo na kiwanda ningeweza kuuza nyanya zote na kupata faida, lakini sasa hata gharama zangu sidhani kama zinaweza kurudi,” anasema.

Mkulima huyo anasema, gharama za shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja zilikuwa Sh. 1 milioni na kwamba alipovuna alipata jumla ya matenga 80, lakini matenga 30 yalionekana yameharibika tangu shambani huku mengine 20 yakiharibika wakati alipozifikisha nyanya hizo kwenye soko dogo kando ya mto huu.
Bei ya soko ambayo aliikuta kwa siku hiyo ilikuwa Sh. 5,000 tu kwa tenga moja, hivyo kujikuta akiambulia Sh. 150,000 kwa matenga yake 30 ambayo yalionekana yanafaa kusafirishwa.
Jacob ni miongoni mwa wakulima wengi wa Mkoa wa Iringa wanaojishughulisha na zao la nyanya ambao wamekuwa wakipata hasara kila mwaka kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.
Inaelezwa kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya zao hilo la nyanya, ambalo ndilo kuu la biashara mkoani Iringa, inaharibika kutokana na ukosefu wa soko na miundombinu bora, hasa barabara.
Wakulima ndio wanaoathirika zaidi licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo.
Hali hiyo imewafanya wakulima wengi kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini, huku wengine wakipunguza ukubwa wa mashamba yao ama kutolima kabisa kutokana na kukosa uwezo wa kuyahudumia.
Maulid Kiboma ‘Papara’, mfanyabiashara wa nyanya, anasema kwamba nyanya inayoharibika ni kiasi kikubwa zaidi kuliko inayofika sokoni.

“Nyanya ikifika hapa sokoni kutoka shambani kiasi kikubwa inakuwa masalo, hivyo inabidi ichaguliwe na iliyo bora ndiyo inayosafirishwa.
“Kabla ya kufika hapa sokoni mkulima anakuwa ameichambua na kuyaacha masalo shambani, lakini ikishachambuliwa tena hapa, hata kama ana matenga 10, anaweza kujikuta amebaki na manne tu ambayo ndiyo yananunuliwa na sisi wafanyabiashara,” anasema Papara.
Papara anasema, wafanyabiashara pia wanapoifikisha nyanya hiyo kwenye masoko makubwa, hasa Dar es Salaam, wanalazimika kuichambua, hivyo kiasi kinachobakia kwa ajili ya matumizi kinakuwa kidogo zaidi ya kilichozalishwa.
Anaongeza kwamba, wakati mwingine bei katika soko la Dar es Salaam inaporomoka kiasi kwamba hata wafanyabiashara wenyewe huamua kutonunua zao hilo kwa ajili ya kusafirisha kwa kuhofia kupata hasara.
“Mwaka huu bei ya tenga moja kwa huku vijijini ilifikia hadi Sh. 2,000, lakini wakati huo soko la Dar es Salaam linakuwa limeshuka hadi Sh. 10,000, bei ambayo ni hasara kwetu,” anasema Papara.
Mfanyabiashara huyo anasema, bei inaposhuka katika masoko makubwa inakuwa hasara zaidi kwao wafanyabiashara wa kati, ambapo hata wakipewa nyanya hizo bure na wakulima hawawezi kuchukua.
“Gharama ya kusafirisha tenga moja, kabla ya manunuzi, ni Sh. 10,000, sasa nikinunua hapa tenga moja kwa Sh. 5,000 na nikakuta bei ya sokoni ni Sh. 15,000 nakuwa nimekula hasara, lakini inakuwa hasara zaidi kwa mkulima ambaye hana mahali pa kupeleka,” anaongeza.
Papara anasema, suluhisho pekee litakalomkomboa mkulima ni kujenga kiwanda cha kusindika matunda na mboga mboga ili wakulima waweze kuuza nyanya zote na kukuza kipato chao.
Anasema kiwanda pekee cha Dabaga kilichoko Iringa mjini hakitoshelezi, hivyo kuitaka serikali na wadau wengine wa maendeleo kufikiria namna ya kuwakomboa wakulima hao.
Masoud Said, mfanyabiashara wa nyanya kutoka Dar es Salaam, anasema serikali, pamoja na kufikiria kujenga kiwanda, lakini pia ijenge masoko ya uhakika vijijini ambayo yatawafanya wakulima wawe na mahali pa kupeleka bidhaa zao badala ya eneo la sasa lililoko katikati ya vijiji vya Iyayi na Uhominyi katika Kata hiyo ya Image.
“Walikuja hapa watu sijui wa Techno Save, wakajenga kijibanda kidogo pale Iyayi kwamba ndilo soko. Pale wamewachezea tu wananchi na kutafuna bure fedha za mradi kwa sababu nyanya zinazozalishwa kwenye maeneo haya ni nyingi kuliko kijibanda kile.


“Jambo jingine ni kujenga barabara imara ambazo zitapitika katika majira yote, tofauti na sasa ambapo barabara ya kutoka Ilula hadi huku Image iko kama mgongo wa mtumbwi kiasi ambacho magari mawili hayawezi kupishana,” anaongeza Masoud.
Martin Kazingumu Kutika, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Image, akizungumzia changamoto ya soko la nyanya, alisema inawatesa wakulima wengi, ingawa juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali kuboresha mazingira ya soko hilo.
“Nyanya nyingi zinaharibika japokuwa wakulima wanakuja huku kuzifuata. Bei nayo inapanda na kushuka kiasi kwamba ni vigumu kwa mkulima kunufaika moja kwa moja,” anasema.
Anaongeza kwamba, kujengwa kwa soko katika Kijiji cha Iyayi kutapunguza kero kwa wakulima na wafanyabiashara, kwani eneo lililopo soko la sasa siyo rasmi na linamilikuwa na Shule ya Msingi Uhominyi.
Kaimu Katibu Tarafa wa Tarafa ya Mazombe, Anania Bena Mwangailo, anasema masoko ndiyo changamoto kubwa kwa wakulima ingawa wanajitahidi kuzalisha nyanya.
Mwangailo anasema, katika kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu, tarafa hiyo inayoundwa na Kata za Ilula, Image, Irole, Uhambingeto, Nyalumbu, Lugalo, Mlafu na Ibumu, ilizalisha jumla ya tani 4,473.2.
Hata hivyo, anasema kiasi hicho ni kile ambacho kilipitia katika Soko la Ilula, lakini akasema kiasi kingine kikubwa kinasafirishwa moja kwa moja na wafanyabiashara wanaonunua huko vijijini na kupeleka Dar es Salaam.
“Ni kweli nyanya nyingi zinaharibika huko vijijini kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika na kuyumba kwa bei ya zao hilo, lakini kama kiwanda cha kusindika mazao ya mbogamboga kingekuwepo naamini kilio hiki kingekwisha,” anasema.
Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni, anakiri kuongezeka kwa uzalishaji wa nyanya mkoani humo, ambapo anasema kwa msimu wa 2011/2012, jumla ya hekta 6,817 zililimwa kwa umwagiliaji na tani 115,514 zilivunwa.
Hata hivyo, anasema changamoto ya masoko inaendelea kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga masoko madogo vijijini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama mashirika ya TechnoServe, Muvi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).
Anasema kujengwa kwa masoko hayo kutawawezesha wakulima kufikisha mazao yao mahali pamoja na kujua bei inayozunguka sokoni, hivyo kuwaepusha na walanguzi ambao wanawapunja.
“Kuna mwekezaji mmoja ambaye alikuwa amejitokeza kutaka kujenga kiwanda katika Kijiji cha Viwegi, ingawa sijajua amefikia hatua gani, lakini naamini kikijengwa kitasaidia uchumi hasa kwa zao la nyanya ambalo kwa kweli linategemewa na wakulima wengi mkoani Iringa,” anasema.

CHANZO: KWANZA JAMII-IRINGA

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: