Home > All Stories > Takukuru inapokuwa ‘mbwa wa kulinda maslahi ya wakubwa’

Takukuru inapokuwa ‘mbwa wa kulinda maslahi ya wakubwa’

 

‘MHARIRI wa gazeti la Rai kizimbani kwa rushwa’. Hii ni habari iliyopamba kurasa nyingi za mitandao ya kijamii zikizungumzia sakata la Mhariri wa Habari wa gazeti kongwe la Rai, Masyaga Matinyi, kwamba alikamatwa na rushwa huko Monduli, mkoani Arusha.

Japokuwa siyo vyema kuingilia kati uhuru wa Mahakama, lakini mtaniwia radhi Watanganyika wenzangu nikiichukulia mfano kadhia hii, kwa sababu inawahusu wanahabari wenzangu kote ulimwenguni.

Sitaki kuingia kwa undani zaidi katika kadhia hiyo, lakini nataka kuainisha baadhi tu ya mambo machache ambayo binafsi yananitia mashaka kuhusiana na ukweli ama uongo wa kuomba na kupokea rushwa kwa mwanahabari huyo makini nchini.

Namfahamu vizuri Masyaga Matinyi, na hata kaka yake ninayemheshimu sana, Mobhare Matinyi aliyeko Marekani kwa sasa. Sijawahi kufanya nao kazi ofisi moja, lakini kama wanahabari, tumekuwa tukigongana kila wakati mitaani ‘tunaposaka nyoka’.

Kadhia nzima iliyomkumba Masyaga na wenzake ni kiinimacho. Simtetei na sitathubutu kumtetea mkosefu hata siku moja, lakini katika hili nitasimama daima kutetea haki, ingawa naamini kabisa kwa wahusika wa Takukuru ‘nitakuwa nimewatangazia vita’, sijali.

Sakata la ufisadi wa kigogo wa Tanesco Monduli, Andrea Meza, lilikwisharipotiwa muda mrefu, kwa kumbukumbu zangu ni tangu mwishoni mwa mwaka 2011. Juhudi za kukanusha na kutaka kujitakasa watakasike zimefanyika bila mafanikio, hasa ikizingatiwa kwamba, Tanesco ni taasisi ya umma na sote lazima tushiriki kulinda ustawi wake.

Kwa kipindi kirefu, Andrea Meza, amekuwa akilalamikiwa na jamii kwa kujihusisha na ufisadi wa magogo ya miti ya stimu na ndilo tatizo lililowapeleka akina Masyaga kwake pamoja na suala la sifa zake zilizompa nafasi ya msimamizi wa mafundi wa Tanesco Monduli.

Kama kuna wanahabari waliopotoka, ambao wanageuza uzembe wa watendaji wa umma kama kitegauchumi chao cha kuvuna fedha haramu, hao siwatetei, japokuwa naamini kwamba wapo kwa sababu ‘Safari ya Nzige na Panzi wamo!’

Japokuwa sikuwepo Monduli, lakini kwa mazingira ninayoyafahamu kama mwanahabari mwandamizi nchini, na kwa uzoefu wangu wa miaka 20 kwenye tasnia ya habari, naamini Masyaga alikwenda Monduli kwa nia njema kabisa ya kujiridhisha kuhusu kashfa hiyo.

Kwa kutambua maslahi ya umma, na pengine kwa kujua kuna umuhimu wa kupata ukweli, ndiyo maana alilazimika kufunga safari hadi Monduli ili apate ukweli huo.

Narudia tena, mawazo yangu haya yasichukuliwe kama kuingilia uhuru wa Mahakama (Contempt of Court). Kama Mtanzania ninayo haki ya kueleza vile nionavyo na hasa katika kipindi hiki ambacho taasisi nyingi za umma zinaficha taarifa kwa sisi wanahabari na inapotokea kigogo kakumbwa na ufisadi, anatafuta namna nyingine ya kuwanyamazisha waandishi.

Haiingii akilini hata mara moja kwa Masyaga kufunga safari kutoka Dar es Salaam kufuata Sh. 200,000 Monduli. Hapo kuna namna.

Siwezi kuamini kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekosa watu makini wenye uwezo wa kutafakari na kutathmini mambo kwa kina badala ya kukurupuka na kuweka mitego ya kitoto kama walivyofanya.

Tumezaliwa na kukulia katika misingi ya Tanu inayosema ‘Rushwa ni adui wa haki, Sitapokea wala kutoa rushwa’, hivyo nafahamu hata kuanzishwa kwa Takukuru kulikuwa na maana nzuri ya kuunda chombo kitakachopambana na yeyote mwenye kwenda kinyume na kauli hiyo pamoja na Katiba ya nchi.

Tukio la kukamatwa kwa Masyaga limewakumba wanahabari wengi nchini Tanzania. Kama nilivyotangulia kusema, simtetei yeyote anayevunja sheria, hivyo ninaamini wapo ambao walistahili kukamatwa kwa sababu yawezekana kweli waliomba na wakapokea, wengine hata wakashinikiza. Wapo, tena wengi tu.

Kigogo huyo wa Tanesco siyo wa kwanza kushiriki mchezo mchafu wa kuwakamatisha waandishi kwa rushwa. Wapo wengi tu, na wamefanya kama ndio utaratibu wao.

Kwa jinsi ilivyo siku hizi, vigogo wengi wamebuni utaratibu mbovu wa kuwadhibiti wanahabari pindi wanapobaini kwamba wamefanya madudu kwenye idara wanazoziongoza.

Njia iliyo nyepesi zaidi ni kuwalaghai kwamba waende wakamalizane nao ili mambo yaishe, lakini wakati huo huo wanawasiliana haraka na Takukuru kwamba kuna mwandishi mmoja anamsumbua akitaka kupewa rushwa, hivyo waweke mtego kwa kumnasa, bila kueleza ukweli kwamba yeye amefisidi mali ya umma na anataka kutumia njia hiyo kuzima kashfa yake.

Baadhi ya maofisa wa Takukuru wasio waadilifu, ambao nao wanatumia chombo hicho kama kitegauchumi chao, wanashiriki mchezo huu mchafu bila kufikiria. Zaidi wameelekeza nguvu zao kwa wanahabari huku nao pia wakihofia kuumbuliwa kwa madudu wanayoyafanya.

Kama ambavyo wananchi wamekuwa wakililalamikia Jeshi la Polisi nchini kwamba baadhi ya askari wamekuwa na kawaida ya kuwabambikia raia kesi, ndivyo ambavyo Takukuru wanafanya hivi sasa. Sijui kama mtani wangu Edward Hosea analifahamu hili.

Watumishi wengi wa umma, hasa wenye dhamana ya uongozi katika idara na taasisi, wamekosa uzalendo wa kweli na kugeuza ofisi hizo chemchemi za kuvuna mahali wasipopanda, bila kujali maslahi ya umma.

Hivi sasa hawaoni haya kabisa, wanachofanya ni kuwasiliana na maofisa wadogo wa Takukuru, ambao nao – nasikitika kusema ni ‘wala rushwa’ – na kuweka mitego ya ajabu ambayo mwisho wa siku inaonekana kuwabambikia kesi watu wasiostahili na kuwaacha mafisadi wakiendelea kupeta.

Unategemea kigogo huyo atafanywa nini kama mwanahabari aliyekuwa akifuatilia kashfa amekamatishwa rushwa kwa nguvu? Hiyo inaleta taswira ya hofu na woga kwa wanahabari wengine kumfuata kigogo huyo kwa kuogopa kwamba nao wanaweza kukamatishwa rushwa.

Takukuru hii ambayo wakati inaanzishwa wananchi walikuwa na imani nayo, sasa haitendi haki, badala yake imekuwa kama ‘Mbwa wa wakubwa’, maofisa wake wengi wasio waadilifu wakitumika kuwalinda wakubwa na kashfa zao ili yeyote, hasa wanahabari, atakayejitokeza adhibitiwe haraka.

Takukuru hii, ambayo tunaamini ndiyo ilipaswa kuwa ya kwanza kutambua hata mikataba mibovu inayoigharimu Serikali kwa sasa, imekuwa kama tembo wa karatasi ikiiacha nchi ikiingia kwenye gharama kubwa na baadhi ya maofisa wake wakikimbilia kuwadhibiti wanahabari wanaowafuatilia watendaji wa serikali wasio waadilifu.

Inashangaza kuona ufisadi ukifanyika nchini kwa miaka mingi hadi Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aje agundue ufisadi huo. Takukuru wapo, lakini wanafanya nini? Kukimbilia kuwakamata akina Masyaga na wenzake?

Takukuru watambue kwamba, wanatumia kodi zetu kulipana mishahara minono, posho na masurufu mengine kede kede, lakini badala ya kushirikiana na wanahabari, wao ndio wanakuwa ngao ya mafisadi kuzuia ufisadi usianikwe.

Taasisi nyingi za umma zimeoza kwa ufisadi, kuanzia Tanesco, TRA, Tanroads, Ewura, TCRA na sehemu nyinginezo, achilia mbali vyombo vya dola na vile vinavyostahili kutoa haki, hasa mahakama. Lakini hakuna ambacho kimefanywa na Takukuru kupambana rushwa hiyo.

Kinachofanyika ni kama mchezo wa kuigiza tu, kwa sababu ukiangalia utakuta watoa rushwa na wapokea rushwa wakubwa hawaguswi. Ukienda mahakamani utakutana na kesi za makabwela waliokamatwa kwa rushwa ya Sh. 10,000 huku waendesha mashtaka wa Takukuru wakkiwa wametokwa mishipa shingoni na mate kuwakauka.

Kasi waliyonayo katika ‘kesi za kutengeneza’ dhidi ya wanahabari na makabwela wengine kama ingekuwa ikitumika kushughulia mambo mengi yenye maslahi kwa taifa letu, hakika tungeweza kuitendea haki nchi yetu tofauti na sasa.

Kwa kifupi, Takukuru haiko huru, haina nia madhubuti ya kupamaba na rushwa ikiwa mwenendo wake ni huu wa kuweka mitego ya kuwanyamazisha wanahabari, hivyo kuleta taswira kwamba ni chombo cha kuwalinda wakubwa, hata kama wameoza kwa ufisadi.

Wanahabari ndio wamesaidia kuibuliwa kwa mambo mengi ya ufisadi, lakini mafisadi, kwa kuhofia vitumbua vyao kuingia mchanga, wanafanya kila jitihada kuwanyamazisha – kwa njia halali na haramu. Huu siyo uwajibikaji wa chombo makini kama Takukuru.

CHANZO: KWANZA JAMII-IRINGA JUNI 27, 2012

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: