Home > All Stories > Kutoka mwindaji wa Ethiopia hadi Chifu wa Wahehe

Kutoka mwindaji wa Ethiopia hadi Chifu wa Wahehe

Hili ni kaburi la Mtwa Munyigumba Kilonge Mdegella Mwamuyinga lililo katika Kijiji cha Rungemba wilayani Mufindi, takribani kilometa 61 kutoka Iringa mjini.

Na Daniel Mbega

MAANDIKO kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.

‘Jicho halishibi kuona na Sikio halikinai kusikia!’ hivyo nikaamua kufunga safari hadi Lungemba, yaliko makaburi ya Mtwa Munyigumba na ndugu wengine wa ukoo huo, yapata kilometa 62 kutoka Iringa Mjini.

Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija, lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.

Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad. Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa na mwanamke wa Kikaguru. Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila, kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo inatoweka kutokana na Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.

Rungemba ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia kama lilivyo jina la Mkwawa, lakini hapa ndipo kwa kiasi kikubwa lilipo chimbuko la Chifu huyo wa kabila la Wahehe na ndipo lilipo kaburi la Mtwa Munyigumba.

Ignas Pangiligosi Muyinga, maarufu kama Malugila Mwamuyinga (61), ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, anaona fahari kuisimulia historia ya ukoo huo maarufu.

“Shina la ukoo wetu linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia,” Malugala anaanza kueleza. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamududa. Wengi walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.”

Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.

‘Vanyategeta’ wao walioishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa),Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.

Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamududa aliyeipenda mno kwa ladha yake.

Alipendwa na kukaribishwa na Mwamududa kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa. Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).

Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.

Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.

“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Malugila.

Muyinga Mfwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume – Maliga, Nyenza na Mpondwa. Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.

Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa.

Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.

Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na Magohaganzali.

Hili ni kaburi la Mtwa Msengele Kilekamagana Munyigumba Mwamuyinga, mdogo wake Mtwa Mkwawa kwa Mama Sengimba mdogo. Picha zote na Admin.

“Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni Kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe), ambapo kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo, ingawa nasikia pembe zile ziliibwa na tunaambiwa walioiba wote walikufa ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na kuzichimbia ili iwe kumbukumbu,” anasimulia Malugala.

Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema, Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.

“Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.

“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea,” anaeleza Malugala.

Malugala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.

Inaelezwa kwamba, alipomfukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.

“Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao,” anaeleza.

Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagala; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.

Advertisements
Categories: All Stories
 1. R. J. Kahwa
  July 11, 2012 at 9:59 am

  Shirikiana na hao ndugu walio hai kuandika kitabu kitakachoweka kumbukumbu ya kudumu.

 2. Mussa Omary
  July 11, 2012 at 2:04 pm

  Duh, kwani ndiyo mwisho wa story it is very interesting

 3. Kitova
  July 11, 2012 at 6:12 pm

  Nimeipenda hii historia, na kazi nzuri uliyojitahidi.
  Jina la Kitova naona hii ni mara yangu ya kwanza kuisikia hii tafsiri yake. Mimi naijua ya mpigaji mwenye shabaha zaidi

 4. Mathan Laiseck Chalamila
  September 18, 2012 at 7:06 pm

  BELA UFANYILE IKASI NOFU,
  MAANA ISIKU ISI ULUKOLO LWIYAGA KWA KUVAA SITWISELI NDA

 5. Yuward Mhapu
  December 12, 2012 at 6:39 pm

  Nimeipenda sana hii historia ,Lakini endelea kufanya utafiti zaidi ili kama ikiwezekana kiandikwe kitabu ili kuitunza historia hii muhimu.

 6. RICHARD Y .KHAGODA
  January 25, 2013 at 7:30 am

  Aah, umemiudhi nilikuwa natiririka na story, inafurahisha sana…. umeikatiza ghafla
  . endelea na utafiti wako tuleteee mambo yaliyojiri. lakini umenisisimua sana.

 7. HAMAD ADAM MUYINGA MKWAWA
  January 5, 2014 at 11:40 am

  UYEPE HILO ULUKANI ULU NENE NDITIGILA WANDIKE MUMAKARATASI TUGULA

 8. robert tossi
  April 23, 2015 at 9:48 am

  waweza fikiri ni kitu chepesi, lakini umefanya jambo muhimu mno mno mno, bog up, yaani umewasha moto ndani yangu wa kufanya na kuishi utafiti, naumia, historia yetu inapotea, kwanza kama watanzania pili kama wahehe. Ndilumba mulugu..

 9. JUSTINE GALAKWILA MKINI
  March 16, 2016 at 12:47 am

  Iko poa sana,,,maana baada ya kusoma kwangu nikagundua kuwa MWAMKINI nipo hapo

 10. March 16, 2016 at 1:05 am

  iko poa sana,Maana nimesoma na nimepata kugundua kuwa ukoo wangu wa MKINI ni kizazi cha MALIGA………..Tusije tukajisahau na kuanza kuoana…ukoo wote upo hapo na tuwe makini wakina MUYINGA wenzangu.

 1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: