Home > All Stories > Maliga: Kizazi cha nne cha Daktari wa Chifu Mkwawa

Maliga: Kizazi cha nne cha Daktari wa Chifu Mkwawa

Na Daniel Mbega
KWA Jangwa Maliga (38), mkazi wa Kijiji cha Image katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, kutibu majeraha na mifupa iliyovunjika kwa ajali umekuwa utamaduni wake wa kila siku.
Kwake kuchelewa kulala ama kuamshwa usiku wa manane ili awahudumie majeruhi hao siyo karaha, kwani amekuwa akiifanya kwa miaka 13 sasa mfululizo.
Maliga, ambaye hakuwahi kuliona darasa la tiba za kisasa, amekuwa mkombozi na kimbilio la wahanga wengi wa ajali, ambao ama wamepata majeraha makubwa yaliyoshindikana kupona au kuvunjika mifupa ambayo imeshindwa kuungwa katika hospitali kubwa.
Hana x-ray, hana utaalamu wa kisasa, lakini anasema anaweza kumtazama mgonjwa na kujua tatizo gani linalomsumbua na tiba ipi ambayo itamsaidia mpaka apone.


“Sijasomea tiba hii, lakini hata nikikaa na madaktari bingwa nitawaeleza kwa Kiswahili tatizo linalomsumbua mgonjwa, maelezo ambayo hayawezi kuwa tofauti na watakayoyatoa wao kwa lugha ya kitaalam.
“Naangalia aina ya majeraha yenyewe, kama ni mfupa wa fibula, tibia, femur, radius, ulna au humerus umevunjikaje. Wachache, ambao matatizo yao yanakuwa makubwa, huwa nawaeleza moja kwa moja tu kwamba hakuna jinsi inabidi wakakatwe viungo vyao,” anasema.
“Wagonjwa wengine wanakuja hapa wakiwa wamekata tamaa baada ya muambiwa na madaktari bingwa huko hospitali kwamba mifupa yao haiwezi kuungwa, inabidi wakatwe, lakini kwa uwezo wa Mungu, wakija hapa wanasimama na kutembea,” ndivyo anavyoanza kueleza mtaalamu huyo wa kutibu mifupa kwa kutumia dawa asilia.
Anaeleza kwamba, japokuwa wapo majeruhi wa ajali za magari, lakini wengi wanaokwenda kwake ni wale wa ajali za pikipiki (bodaboda), hasa kutoka vijijini ambako usafriri ni wa shida.
Wengine, anasema, miguu ama mikono yao iliyovunjika inakuwa imevunda kutokana na kuumia na kukaa muda mrefu bila tiba, lakini anajitahidi kuwatibu na wengi wanapona.

Ni hospitali…
Nyumbani kwake kumekuwa kama hospitali, kwani umati wa watu utakaokutana nao ukiwa ama umepanga foleni kumsubiri au kuhudumiwa na vijana wanaomsaidia kazi unatosha kumwelekeza mgeni yeyote kwamba hapo kuna shughuli inayoendelea.
Tatizo kubwa lililopo ni kwamba, nyumba yake haitoshi kuwahifadhi watu wengi, ingawa mwenyewe anasema wakati mwingine analaza wagonjwa hadi 40 kwa wakati mmoja.


“Kwa wiki wanakuja wagonjwa 10 hadi 20, wengine wanakuja hawawezi kutembea, lakini baada ya wiki moja hadi mbili wanasimama na hatimaye wanatembea,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema, kutokana na uhaba wa nafasi nyumbani kwake, wagonjwa wengi pamoja na ndugu wanaowasindikiza wanalazimika kupanga katika nyumba za jirani huku wakiendelea na tiba.

Changamoto
Pamoja na kutoa huduma hiyo muhimu kwa jamii, Maliga anasema changamoto zinazomkabili ni nyingi, lakini awali ya yote ni kukosa nafasi ya kuwahifadhi wagonjwa kutoka na nyumba yake kuwa ndogo.
“Nimejitahidi kukusanya fedha kidogo zinazochangwa na wagonjwa wenyewe kwa ajili ya tiba ili kukarabati nyumba hii kwa kuisakafia, angalau sasa wanaweza kutandika hata mikeka na kulala,” anasema.
Changamoto nyingine ni kwa baadhi ya wagonjwa kutokuwa na fedha za kulipia matibabu. “Hali hii inanifanya nishindwe kutoa huduma kwa wagonjwa wengine kwa sababu hiyo ndiyo fedha ninayotegemea kwa ajili ya kwenda porini kuchimba dawa nyingine.”
Michael Kisina, mkazi wa Mafinga, ni miongoni mwa wagonjwa waliopo nyumbani kwa Maliga wakipatiwa tiba baada ya kuvunjika mguu tangu Machi 2012 kufuatia ajali ya pikipiki.
Anasema juhudi za kupata tiba katika hospitali za serikali, ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Iringa, zilishindikana, lakini tangu afike hapo wiki mbili zilizopita, hali yake inaendelea vizuri.
“Hali yangu ni tofauti na nilivyokuja, nashukuru kidonda kimeanza kupona na hata maumivu ya mguu kwa ujumla yanapungua, japokuwa sijaanza kukanyaga,” anasema.

Alikoupata utaalam
Maliga anasema utaalam wa tiba asilia za mifupa ni wa vizazi na vizazi, kwani ameurithi kutoka kwa baba yake, Moses Maliga (83), ambaye kwa sasa amestaafu kutokana na umri.
Anasema babu wa baba yake, ambaye ndiye mwenye jina la Maliga, ni wa ukoo wa Munyigumba, baba yake Chifu Mkwawa, hivyo yeye ni kizazi cha nne cha Maliga.
“Huyo babu yetu Maliga ndiye aliyekuwa akitibu majeruhi wa vita wakati Mkwawa alipokuwa anapambana na Wajerumani, lakini baada ya Chifu Mkwawa kujiua mwaka 1898, babu akakimbilia eneo la Dabaga na kujificha huko akihofia kukamatwa,” anasimulia.
Hatimaye babu yake alihamia Image, ambako ndiko walikoweka maskani mpaka sasa, lakini mawasiliano na ndugu wengine wa ukoo wa Munyigumba yameonekana kukatika.
Hata hivyo, anasema kwamba, tangu wakati huo kizazi hicho cha Maliga kimeendelea kutibu majeruhi wa ajali tu wenye matatizo ya mifupa.
“Nilianza kufundishwa tiba hii tangu mwaka 1986 nikiwa shule ya msingi, ambapo baba alikuwa akinituma kuchimba dawa na kunielekeza namna ya kuchanganya dawa hizo,” anasimulia Maliga, ambaye ndiye pekee aliyefundishwa tiba hiyo kabla naye hajamfundisha mdogo wake.
“Lakini katika kipindi hicho chote, baba alikuwa akinisisitiza kwamba, dawa hizo hazitibu mifupa inayoanza tu kuuma, isipokuwa kwa watu waliopatwa ajali pekee. Hatupigi ramli, wala hatutibu magonjwa mengine hapa,” anaongeza.
Huu ni utamaduni, jadi yetu ya Kiafrika iliyotumiwa na mababu zetu miaka nenda rudi, ambayo imeendeleakuwa mkombozi na kimbilio la wengi hata pale tiba za kisayansi zinaposhindika.
Ni kweli kwamba zipo mila potofu, lakini mila na tamaduni nyingine kama hizi zinapaswa kuenziwa, ikibidi wahusika wanaoendesha shughuli hizi kama Maliga, wapewe msaada na Serikali na jumuiya nyingine ili kuboresha huduma zao.

Advertisements
Categories: All Stories
 1. Shanifa
  July 12, 2012 at 11:25 am

  Asante sana kwa kumpata ndugu yetu anayeweza kutibu mifupa katika ajali zetu za mabarabarani. Mimi pia ni mnyalu wa huko huko kilolo, je ninaweza kusaidiwa kupata namba za simu za Maliga, kwakuwa huku niliko mimi Dar Es Salaam tunao majirani, ndugu zetu wanashindwa pa kupata tiba ya bei rahisi kama hiyo ya kaka.

  Tafadhali naomba Namba za simu ndiyo muhimu.

  Ubarikiwe sana,

  Ndugu yako,

  Shanifa Duma.

 2. HAMAD ADAM MUYINGA MKWAWA
  January 5, 2014 at 11:59 am

  hongera maliga. endelea kutoa huduma hiyo hata mdogo wanu wiliad lutego ameponea kwako baada ya kuhangaika zaid ya mk 2 hsal

 1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: