Home > All Stories > Utawala wa Munyigumba wapinduliwa na mkwewe

Utawala wa Munyigumba wapinduliwa na mkwewe

Na Daniel Mbega
UTAWALA wa Munyigumba Kilonge Mwamuyinga ulidumu kwa muda wa miaka 19 tangu alipomuua kaka yake Ngawonalupembe mwaka 1860.
Mtwa Munyigumba alifariki mwaka 1879 katika Kijiji cha Lungemba akiwa amefanikiwa kuziunganisha koo zaidi ya 100 ambazo baadaye ndizo zilizozaa kabila la Wahehe, wakati Munyigumba anafariki, Mtwa Mkwawa, ambaye ni mtoto wake wa kwanza, alikuwa na umri wa miaka 24.
Kutokana na umri mdogo wa Mkwawa, ikabidi asikabidhiwe kwanza uchifu kwa wakati huo, hivyo ukoo ukamteua mdogo wake Munyigumba, Mtwa Mhalwike, aliyezaliwa na mke wa tatu wa Mtwa Kilonge, Mama Sekindole.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya Mtwa Munyigumba kufariki na kutawazwa kwa Mhalwike, utawala huo ukapinduliwa na mmoja wa wafuasi wake na pia mkwewe aliyekuwa amemuoa binti yake. Mtu huyo, Mwamubambe Mwalunyungu, alikuwa anatokea eneo la Wassa na enzi za utawala wa Munyigumba ndiye hasa aliyekuwa kitumwa kazi ndogo ndogo kiasi cha kupendwa na hatimaye akapewa binti wa Chifu.
“Huyu Mwamubambe kwa nini mdogo wake Munyigumba atawale? Nchi hii nitaichukua mimi mwenyewe,” anasimulia Malugala Mwamuyinga, mjukuu wa Msengele Kilekamagana, ambaye ni mdogo wake Mkwawa.
Mwamuyinga anasema, Mwamubambe alimvia Mhalwike kichakani, akampiga na kumchinja katika eneo hilo la Lungemba. Alipomaliza kazi yake hiyo haramu akaenda mahali ambako watu walikuwa wanakunywa pombe na kusema: “Nchi hii ni yangu. Kama mnabisha nendeni kule kwenye miti mkamtazame Mhalwike.” Walipokwenda huko wakakuta maiti ya Mhalwike ikiwa imechinjwa kama kuku.
Wakati huo Mtwa Mkwawa alikuwa bado mdogo sana kupewa madaraka na kwa vile tayari Mwamubambe alikuwa ameupindua utawala, wakahisi Mtwa Mkwawa angeweza kuuawa kwa sababu ndiye mtoto mkubwa wa Munyigumba na ndiye hasa aliyetarajiwa kutawala. Hivyo, ikabidi wamkimbize kwenda kumficha Dodoma kwa Mtemi Mazengo wa Wagogo. Hii ndiyo sababu Wagogo wanawaita Wahehe wajomba zao na wanaheshimiana mno.

Mkwawa arejea
Wahehe hawakufurahishwa na utawala wa Mwamubambe anayechukuliwa kama adui mkubwa zaidi katika historia ya kabila hilo kuliko hata Wajerumani. Kwa hiyo basi, wakapanga mbinu za siri kumrejesha Mtwa Mkwawa kutoka uhamishoni.
Mtwa Mkwawa, wakati huo akiwa amejifunza mbinu za juu za kivita, akaamua kurejea na kuunda jeshi lake ili kupambana na Mwamubambe.
Hata hivyo, wapiganaji wengi wa Mtwa Mkwawa aliuawa na Mwamubambe, mtu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa akitumia zaidi mitishamba kushinda vita nyingi kwa sababu hata dawa alizokuwa anatumia ndizo zilizokuwa zikitumiwa na Mtwa Munyigumba, huku Mwamubambe mwenyewe ndiye akielekezwa kuzitafuta porini.
Kutokana na wapiganaji wengi kuuawa na Mwamubambe, wapiganaji wengine walikuwa wakilia na kupiga kelele; “Hee Hee Hee! Mtwa tuisila!” wakimaanisha; “Hee Hee Hee! Mtwa tunakwisha!” Hapa hasa ndipo lilipoanza jina la kabila la Wahehe kutokana na kelele walizokuwa wakizipiga.
“Wafuasi wake walikuwa wanakufa sana. Siku moja Mkwawa akajiwa kwenye ndoto na baba yake Munyigumba ambaye alimwambia kwamba hilo jitu hawataliweza. Lilikuwa likichomwa mikuki linachomoa na kuwarushia wao na kuwaua,” anasema Malugala Mwamuyinga.
Inaelezwa kwamba, Munyigumba alipomtokea Mkwawa kwenye ndoto akamwambia, roho ya Mwamubambe iko kwenye kidole au kwenye kisigino. Hata wakifanya namna gani hawawezi kumuua. Hivyo akamtaka amtafute Mkimayena Mwakinyaga amwambie akamchome Mwamubambe kwenye kisigino au kidole.

Lundamatwe
Mwamubambe alikuwa na jeshi kubwa na wafuasi wengi wenye uwezo wa vita, Mtwa Mkwawa akalazimika kujipanga upya ili kuwapiga na kuyarejesha maeneo yote yaliyokuwa yametwaliwa na Mwamubambe.
Mapambano makali kabisa ya Mkwawa na wafuasi ya Mwamubambe yaliianzia eneo ambalo leo hii linafahamika kama Lundamatwe (Lundika Vichwa), lakini yapata kilometa mbili kutoka Barabara Kuu ya Tanzam upande wa kusini.
Hapa palikuwa nyumbani kwa mganga Ngondo Kimamula Mbugi, pembezoni mwa Mto Ruaha. Inaelezwa kwamba, mganga huyo aliamua kuchukua jukumu la kuwaandaa wapiganaji wa Mkwawa kukabiliana na maadui zake.
Wapiganaji wa Mkwawa baada ya kuganguliwa wakaondoka kupambana na Mwamubambe na wafuasi wake ambapo waliwapiga na kuwaua zaidi ya wapiganaji 1,000.
Mwamubambe alipona mambo yamemzidia akatimua mbio, lakini wapoganaji wa Mkwawa wakaanza kumfukuza.
Kwa vile Mkwawa alikuwa ameelekezwa na baba yake ndotoni kuhusiana na Mwamubambe, akaamua kumtuma Mukimayena Mwakinyaga, ambaye alikuwa mganga wa kienyeji, ili akamuue.
Mwakinyaga akaenda na kumkuta Mwamubambe anakunywa pombe. Mbele ya umati wa watu, akamchoma mkuki kwenye kidole. Mwamubambe akadondoka chini na kuanza kutapatapa bila kukata roho.
“Mwamubambe akamuuliza Mwakinyaga, ‘Umenifanya nini?’ Mwakinyaga akasema, ‘Aah ni mikuki tu’. Basi alipoona mambo yamekuwa magumu, akamwambia; ‘Kaniitie Mkwawa aje’. Mkwawa alipofika Mwamubambe akamwambia; ‘Wakorofi kama mimi wapo wengi ndani ya utawala wako, kwa hiyo sasa ukazane’.
“Kwenye ndoto, baba yake alikuwa amemwambia Mkwawa kwamba akishafika aukite mkuki wake chini. Basi Mkwawa akaukita mkuki chini. Ndipo Mwamubambe akakata roho,” anaeleza Mwamuyinga.
Mwamuyinga anasema kwamba, kwa vile Mwamubambe alikuwa amewatesa na kuwaua Wahehe wengi, baada ya kufa ikabidi, kwa hasira, wananchi wale wamkatekate vipande vipande na kuila nyama yake ili lisiwepo kabisa kumbukumbu lake.
Baada ya hapo Mtwa Mkwawa akaendesha mapambano ya kuyakomboa maeneo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa Munyigumba, kampeni ambayo iliendelea moja baada ya nyingine kwa mafanikio makubwa kuliko hata awali.

Advertisements
Categories: All Stories
  1. HAMAD ADAM MUYINGA MKWAWA
    January 9, 2014 at 5:05 pm

    story hii imenifurahisha sana angalat sasa naweza jua kwa muktasari asili ya muyinga

  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: