Home > All Stories > Mkwawa awatisha Wajerumani

Mkwawa awatisha Wajerumani

Askari wa Kihehe.

Na Daniel Mbega

BAADA ya kufanikiwa kuurejesha utawala kwenye himaya yake mwaka 1890 kufuatia kumtwanga Mwamubambe Mwalunyungu aliyekuwa na walugaluga kutoka Tabora, Chifu Mkwawa aliendelea kuuimarisha utawala huo kwa ujasiri mkubwa akiwazuia Wamasai wasiende kusini pamoja na kupambana pia na biashara ya utumwa iliyokuwa ikiendeshwa na Waarabu.

Wakati huo alikuwa ameimarisha urafiki wake wa kibiashara na Waarabu katika Pwani ya Tanganyika, ambao walimpatia bunduki pekee aliyokuwa akiitumia mwenyewe.

Hata hivyo, mapambano mengine makubwa zaidi yalikuwa yanajongea ambayo yangehitaji ujasiri mkubwa kuyakabili.

Kufikia mwaka 1890 majeshi ya Ujerumani, maarufu kama Wissmanntruppe (Kikosi cha Wissmann), yalikuwa yamefanikiwa kuyashinda majeshi ya upinzani ya Abushiri na kuitwaa Pwani yote ya Tanganyika (wakati huo ikijulikana kama German East Africa). Mnamo mwezi Mei 1891 Kikosi cha Wissmann kilibadili jina na kuitwa Kaiserliche Schutztruppe na von Wissmann akastaafu kwenye jeshi hilo la Afrika akimwachia Luteni Emil von Zelewski kuliongoza.

Njia zote za misafara ya kibiashara ya pwani hazikuwa salama kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa makabila ya maeneo hayo, hususan upande wa kusini wa koloni lao kutoka kwa makabila mashuhuri kwa vita kama Wangoni, Wagogo na Wahehe ambao walipora misafara hiyo.

Wakati huo Wahehe walikuwa wameimarisha himaya yao kutoka Iringa ilikokuwa ngome ya Chifu Mkwawa kuelekea pwani ambako Wajerumani walikuwa wameishikilia. Kutoka kwenye kabila lililotawanyika kwenye miaka ya 1850 chini ya Chifu Munyigumba, sasa Wahehe walikuwa himaya kubwa chini ya Mkwawa.

Wakati wa kiangazi cha mwaka 1891 von Zelewski aliamua kupambana na hali hiyo kwa kutumia nguvu ya jeshi kuanzia Kilwa kuelekea Bara.

Awali Emil von Zelewski alikuwa mwanajeshi wa Kikosi cha 99 cha Jeshi la Nchi Kavu cha Rhineland kabla ya kuhamishiwa kwenye Kampuni ya German East Africa mwaka 1886 na hatimaye kwenye kikosi cha Wissmanntruppe mwaka 1889. Alikuwa amefanikiwa kuongoza kikosi cha  Wissmanntruppe yeye binafsi na kwa kushirikiana na vikosi vya Wissmann katika matukio mengi wakati wakipambana na Abushiri kule Pangani. Alikuwa na uzoefu wa kutosha katika vita na kiongozi makini.

 

Muundo wa jeshi lake

Jeshi la von Zelewski lilikuwa na gadi nne ambazo kila moja ilikuwa na askari 90 walioongozwa na maofisa wa Kijerumani na NCO mmoja. Gadi moja iligeuka na kurudi na kuacha gadi tatu kukabiliana na Wahehe. Gadi namba 5 iliongozwa na Luteni von Zitzewitz akisaidiwa na von Tiedewitz, ambapo ilikuwa na askari kutoka Sudan, Gadi namba 6 iliongozwa na Luteni Tettenborn aliyesaidiwa na Feldwebel Kay na ilikuwa na Wasudani pia, wakati Gadi namba 7 iliongozwa na Luteni von Pirch akisaidiwa na Schmidt ambayo iliundwa na askari wa Kizulu.

Pia kulikuwa na kikosi cha bunduki ambacho kiliongozwa na von Heydebreck akisaidiwa na Thiedemann, Herrich na Wutzer wakati ambapo kitengo cha tiba kiliongozwa na Dk. Buschow na Hemprich.

Jeshi la von Zelewiski lililokuwa na maofisa 17 wa Kijerumani, lilikuwa na vyakula vingi pamoja na ng’ombe wao. Kulikuwa na Wapagazi 170 wa Kiafrika ambao kazi yao ilikuwa ni kubeba mizigo, punda 27, ng’ombe 20 na kondoo na mbuzi 60.

Nguo walizotakiwa kuvaa maofisa wa Kijerumani zilikuwa za khaki na kofia nyeupe ngumu (helmet) ambazo zilikuwa zimeidhinishwa na Ofisi ya Ukoloni jijini Berlin kwa ajili ya Jeshi la Afrika Mashariki mwezi Juni 1891. Lakini nguo hizo zilifika Kilwa mwezi Julai 1891 wakati jeshi la von Zelewiski likiwa limeondoka. Kwa hiyo, von Zelewiski na maofisa wake wa Kijerumani walivaa sare za enzi za Jeshi la Wissmann zilizokuwa na michirizi ya njano mikononi. Wale askari wa Kiafrika walivaa kofia nyekundu za tarbush na sare za khaki.

Wapagazi na watu wengine kwenye msafara huo walivaa nguo kama zilizokuwa zikivaliwa na watu wa makabila mengine wakiwemo Wahehe wenyewe na hawakuwa na kofia wala viatu.

Askari walikuwa na bunduki aina ya Mauser Jägerbüchse 71 pamoja na S71 ambazo pia zilitumiwa na maofisa wadogo wa Kijerumani. Makambanda wao walikuwa na bastola kubwa aina ya 1879 Revolver. Wapiganaji wa Kiafrika wao walikuwa na silaha za jadi ikiwemo mikuki.

Vikosi hivyo, chini ya von Zelewiski, viliondoka Kilwa Julai 22, 1891 vikipitia himaya ya Ngoni Mafiti kuelekea Kisaki hadi Myombo karibu na Kilosa, ambapo viliwasili Lugalo Agosti 16, 1891. Huko njiani vikosi hivyo vilikuwa vimeteketeza vijiji kadhaa na havikukutana na upinzani mkali. Walikuwa wamewaona Wahehe wenye silaha njiani, lakini walikimbia baada ya kuwafyatulia risasi. Hali hiyo inaonekana ndiyo iliyompa ujasiri von Zelewiski wa kusonga mbele akiamini kwamba Wahehe wangelazimishwa kusalimu amri.

 

Jeshi la Mkwawa

Mtwa Mpangile, mdogo wake Chifu Mkwawa, ndiye aliyekuwa kamanda wa jeshi la Wahehe. Ndiye aliyeongoza jeshi hilo katika vita vya Lugalo. Kama ilivyokuwa wa wapiganaji wote wa Kihehe, Mpangile alikuwa na uzoefu mkubwa wa vita ingawa ni vite dhidi ya makabila mengine, lakini siyo kwa jeshi imara lenye mbinu kama la Wazungu.

Tofauti na makabila mengine ya Kiafrika ambayo machifu wao ndio waliokuwa mstari wa mbele, Wahehe walikuwa na mbinu kama za Wazungu kwa kumwacha chifu wao nyuma akiamuru namna ya kushambulia.

Jeshi la Wahehe kwenye vita vya Lugalo lilikuwa na wapiganaji 3,000. Ndilo lililokuwa imara zaidi kulinganisha na makabila mengine yote yaliyolizunguka.

Ushindi dhidi ya makabila mengine ya jirani ulikuwa umewapa ujasiri mkubwa na uzoefu wa vita na kwa hakika walikuwa wamejitolea kuhakikisha wanapambana kufa au kupona kuhakikisha wanailinda nchi yao dhidi ya wavamizi wa kigeni.

Wengi kati ya wapiganaji wa Kihehe walikuwa na mikuki na ngao zilizotengenezwa kwa ngozi kama zile zilizokuwa zikitumiwa na Wazulu. Wengine walikuwa na mashoka.

Chifu Mkwawa alikuwa anafahamu kwamba majeshi ya Wajerumani yalikuwa yanakuja kwenye himaya yake. Taarifa zilikuwa zimemfikia mapema mno na kuifahamu mikakati yao yote. Vijana wake mashujaa waliviona vikosi vya Wajerumani wakati vikikaribia Uhehe na kupeleka taarifa za uwezo wa jeshi hilo la Wazungu, hivyo alikuwa amejiandaa kuwakabili.

 

WIKI IJAYO: Mwanzo wa mapigano, Wajerumani wafyekwa

Advertisements
Categories: All Stories
  1. Blastus gwimile.
    December 24, 2013 at 7:07 pm

    Bela wimsugu yono pede uvawafaulite na shule ya fidudu peufanyite ulukan ulukom na lunofu nda ulo, hwehwe twaitigila ufanyite ulwambolea, ino lwelusige vemuyangu veve humye iktabu hali wigusikise ulye na mapesa igo weliwe.

  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: