Home > All Stories > Mwanzo wa mapigano, Wajerumani wafyekwa

Mwanzo wa mapigano, Wajerumani wafyekwa

HUU ni mfululizo wa Makala ya Uchunguzi kuhusiana na historia ya kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Kilonge Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, kama yanavyoandikwa na Mwandishi Wetu DANIEL MBEGA, ambaye amefanya uchunguzi kwa takriban miezi mitatu sasa katika kuhimiza utalii wa ndani na kuhifadhi historia yetu. Endelea na Sehemu hii ya Tano…

 

WENGI wanaikumbuka Vita ya Maji Maji iliyodumu kwa miaka miwili baina ya Watanganyika na Wajerumani kati ya mwaka 1905 hadi 1907. Kinachofanya waendelee kuikumbuka ni mbinu zilizotumiwa na Mtawala wa Wangindo kule Kilwa, Kinjekitile Ngwale huko kwenye Bonde la Ngalambe alipowapaka na kuwanywesha dawa wapiganaji wake na kuwasadikisha kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.

Utaalamu huo ulisambaa karibu sehemu kubwa ya Kusini mwa Tanzania pamoja na Nyanda za Juu ambapo uliwaongezea ujasiri mkubwa wapiganaji hao waliokuwa wakiitetea ardhi yao isitawaliwe na Wazungu.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba, Chifu Mkwawa na watemi wengine wengi wa wakati huo, pamoja na kuwa na mbinu za kupigana vita, walitumia jadi, kwa maana ya dawa za kienyeji, katika kupanga na kupambana na maadui zao.

Kama ambavyo tunaelezwa katika Vitabu Vitakatifu kwamba, Wafalme wa Israel – tangu enzi za Nabii Musa – walikuwa wanawauliza kwanza Makuhani kabla ya kupanga vita, ndivyo watawala wetu wa Kiafrika walivyofanya nao kwa kuomba miungu yao iwasaidie, hasa wakati huo kwa vile dini ya Kikristo ilikuwa haijaenea.

Kwa kutambua mafanikio ambayo alikuwa ameyapata katika vita dhidi ya Mwamubambe Mwalunyungu na wafuasi wake, Chifu Mkwawa alimtumia pia mganga wa jadi Ngondo Kimamula Mbugi katika timu yake ya kumtabiria nini ambacho kingetokea, kama anavyoeleza kitukuu wa mganga huyo, Robert Gabriel Meza Mwaigoga.

Mwaigoga anaeleza kwamba, wapiganaji wa Chifu Mkwawa walikunywa dawa Lundamatwe, mahali pale pale waliponywea kabla ya kupambana na Mwamubambe, katika eneo linaloelekea Mto Ruaha, takriban kilometa tisa hivi kutoka Lugalo ambako ndiko walikotakiwa kupambana na Wajerumani.

Chifu Mkwawa alikuwa na bunduki moja aliyopewa na Waarabu wakati ule wa Biashara ya Watumwa, lakini wapiganaji wake wote walikuwa na silaha za jadi kama mikuki, kombeo, pinde na mishale na mapanga.

Inaelezwa kwamba, akiwa tayari amepewa siri zote za lilivyokuwa jeshi la Wajerumani chini ya Emil von Zelewiski na silaha walizokuwa nazo, Chifu Mkwawa aliwaeleza wapiganaji wake kwamba, watajipanga vyema katika kingo za bonde ambalo Wajerumani wangepita, lakini hakuna ambaye alitakiwa kushambulia mpaka yeye atakapofyatua risasi ya kuashiria mapambano. Ngondo Kimamula Mbugi alikuwa amewapaka dawa ambazo aliwasadikisha kwamba, hakuna Mjerumani ambaye angeweza kuwaona kabla ya mapambano, na wakati huo Wahehe wangekuwa tayari wamewavamia na kuwashambulia, hivyo hata kama wangefyatua risasi zao zingetoka maji.

Sehemu waliyopita Wajerumani pale Lugalo ilikuwa nyembamba kama mkia, kukiwa na kingo kila upande, hivyo kuwawia vigumu kuweza kufanya mashambulizi ya aina yoyote. Zaidi ya hayo, msitu uliokuwepo ulitoa hifadhi nzuri kwa wapiganaji wa Chifu Mkwawa.

Kosa alilokuwa amelifanya Von Zelewiski, pamoja na uzoefu mkubwa wa vita aliokuwa nao, ni kujiamini kupita kiasi na kutotuma wapelelezi wakachunguze njia na uimara wa jeshi la Mkwawa. Aliamini kwamba, jeshi hilo lilikuwa kama yale mengine aliyoyapiga sehemu nyingine na kwamba huenda Chifu Mkwawa hakuwa na nguvu kama za Abushiri wa kule Pangani aliyepigwa mwaka mmoja nyuma.

Inasimuliwa kwamba, malengo ya Von Zelewiski yalikuwa kwenda kuivamia ngome ya Chifu Mkwawa kule Kalenga, lakini hakujua kama tayari Wahehe walikuwa wamejipanga njiani kukifanya kile ambacho hakuna aliyekitarajia.

Ili kuwazuia Wajerumani wasithubutu kufanya shambulio lolote, Wahehe ambao tayari walikuwa wanafahamu uwezo wa jeshi hilo la maadui pamoja na kulifahamu eneo lote na kupanga ni mahali gani waanze kushambulia, walipanga kuwazuia wasitumie mtindo wao wa nusu duara kushambulia. Kwa kuwa walikuwa wamepata taarifa za Wajerumani walivyopigana huko Pwani, Wahehe walikuwa wamejiandaa kuhakikisha wanakabiliana vilivyo na askari hao.

Awali Wahehe walitaka kufanya mashambulizi katika eneo la Ruaha Mbuyuni ambako Mto Ruaha unakatisha (kwa sasa ndipo ulipo mpaka wa Mkoa wa Morogoro na Iringa), lakini inaelezwa kwamba binamu wa Chifu Mkwawa aliyeitwa Kilonge ambaye alikuwa anashughulikia masuala ya habari na ujasusi, alikuwa ameota kwamba wangeweza kushindwa. Ni yeye ndiye aliyetoa ushauri kwamba mapambano hayo yakafanyike karibu na kijiji cha Lula-Lugalo, mbele ya Mto Mgella.

Mkwawa alikuwa na makamanda wenye nguvu kwenye jeshi lake kama Ngosi Ngosi Mwamugumba, Mtemimuma na kaka yake Mtwa Mpangile, ambaye baada ya kuanguka kwa Kalenga, Wajerumani walimtawaza kuwa ndiye Chifu wa Uhehe mnamo Desemba 24, 1896, lakini akanyongwa Februari 1897 kwa tuhuma kwamba alikuwa akivujisha siri na kumpa Mkwawa.

Mbali ya Wahehe, jeshi la Chifu Mkwawa lilikuwa na wapiganaji kutoka kabila la Wabena, ambao waliwekwa akiba na walikuwa wakilinda Kijiji cha Lula-Lugalo ili kama Von Zelewiski angefanikiwa kupenya kwenye mtego uliowekwa na Chifu Mkwawa, basi wao waweze kupambana na jeshi lake.

 

Wakati Von Zelwiski na vikosi vyake walianza safari ya kuelekea Kalenga saa 12:00 alfajiri, tayari Wahehe walikuwa wamekwishajipanga katika njia ambayo waliamini ndiyo wangepitia. Vikosi vya Wajerumani, kama ilivyoelezwa awali, vilipita katika mstari mmoja kutokana na mazingira ya eneo lenyewe.

 

Wahehe walikuwa wakisubiri tu amri ya kamanda wao, Chifu Mkwawa, ili waanze kushambulia. Majira ya saa 1:00 asubuhi, wakati Wajerumani wakipita kwenye bonde hilo, ofisa mmoja Luteni Zitewitz akaliona kundi la ndege na kufyatua risasi kwa lengo la kupata kitoweo. Mlio huo wa risasi ukaonekana kama dalili za ishara ya kuanza mashambulizi. Baadaye milio mitano au kumi ya bunduki aina ya Shenzi ikasikika. Wahehe nao wakadhani kwamba ndiyo ishara ya wao kuanza mashambulizi wakati vikosi vya Wajerumani havijafika kwenye eneo walilopanga kushambulia. Mamia ya askari wa Kihehe wakavamia kwenye kilima hicho na kuanza kuwashambulia Wajerumani waliokuwa wakipita bondeni, wakipiga kelele zao za vita “Hee hee Twahumite! Hee Heeee!” (yaani “Hee Heee Tumetoka! Hee Heeee!”).

Askari wengi wa Wajerumani walikuwa wanatembea bila kuzikoki bunduki zao na hawakuwa na muda wa kuzikoki, achilia mbali kutengeneza mfumo wa kujitetea kabla ya kushuhudia Wahehe wamewavamia. Muundo wa bunduki aina ya Mauser M71 iliyotengenezwa mwaka 1887 haukuwa unaeleweka vyema kwa askari wengi na walitumia dakika kadhaa kabla ya kuanza kufyatua risasi. Kelele ziliposikika wapagazi wote wakakimbia. Punda waliokuwa wamebeba silaha wakaingia katika Kikosi Namba 5 ambapo askari wengi Wasudani wakaanza kukimbia kuokoa maisha yao.

 

WIKI IJAYO: Von Zelewiski apigwa nyundo

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: