Home > All Stories > Von Zelewiski auawa kwa kupigwa nyundo

Von Zelewiski auawa kwa kupigwa nyundo

HUU ni mfululizo wa Makala ya Uchunguzi kuhusiana na historia ya kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Kilonge Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, kama yanavyoandikwa na Mwandishi Wetu DANIEL MBEGA, ambaye amefanya uchunguzi kwa takriban miezi mitatu sasa katika kuhimiza utalii wa ndani na kuhifadhi historia yetu. Endelea na Sehemu hii ya Sita…

 

HADI wakati huo, tayari von Heydebreck – mmoja wa manusura katika vita hivyo – alikuwa amekwishajeruhiwa na kuanguka akiwa amepoteza fahamu, lakini baadaye aliandika kwenye ripoti yake: “…Mfululizo wa matukio hadi wakati huu ulikuwa umetumia dakika mbili au tatu tu. Nilitambua hilo kabla ya kujeruhiwa, Wasudani tayari walikuwa wamekimbia kurudi nyuma vichakani baada ya kufyatua risasi mara mbili hivi. Mimi na askari wa Kikosi cha Tano tulilazimika kujilinda na kujitetea baada ya kuona Wahehe wakija katika umbali wa hatua 30. Kama sikosei, nilimsikia Sajini Tiedemann akisema alikuwa ameumia kabla hajafyatua risasi. Haikuwa rahisi kuona zaidi ya umbali wa hatua tano msituni kutoka pale njiani. Pia hakuna ambaye aliweza kunusurika kwa sababu Wahehe walikuja kwa kasi… Ni wazi walipanga kutushambulia baada ya kufika katikati msitu. Kuvurugika kwa mipango yao kulichangiwa hasa na kitendo cha Luteni von Zitewitz kufyatua risasi…”

Muanzilishi wa Himaya ya Ujerumani Afrika Mashariki, Carl Peters, baadaye Novemba 23, 1891 alimwandikia Gavana von Soden akisema kwamba, katika mapambano mengine na makabila mbalimbali ya Tanganyika, ilikuwa ni bahati tu kwao kutoweza kupata madhara kama waliyopata Wajerumani pale Lugalo, kwani mafunzo yao ya vita yalikuwa yanalenga zaidi kupigana wakiwa wamejipanga pamoja kwa mbinu maalum. Hawakuwa wamejifunza kupigana kila mtu kwa uwezo wake, bali walitegemea zaidi kushambulia kwa pamoja.

Iliwachukua Wahehe dakika 15 tu (kuanzia saa 1:15 hadi 1:30 asubuhi) kuwafyeka Wajerumani na majeshi yao. Von Zelewiski aliuawa kwa kupigwa nyundo kichwani akiwa amepanda punda wake wakati akijiandaa kuwafyatulia risasi wapiganaji wa Mkwawa. Kabla hajadondoka akachomwa mkuki ubavuni.

Hii ndiyo asili hasa ya jina la ‘Nyundo’ kutokana na kamanda huyo wa Wajerumani kuuawa kwa nyundo!

Kuhusiana na kifo cha Kamanda von Zelewiski, kama Mjerumani Tom von Prince alivyoandika baadaye, “Kama nilivyosimuliwa baadaye… na Wahehe walioshuhudia, alijitetea mwenyewe kwa kutumia bastola yake kubwa na kuwapiga risasi watu watatu, wakati kijana mmoja wa Kkihehe alipomchoma na mkuki ubavuni. Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu na alizawadiwa ng’ombe watatu na Mkwawa kwa kitendo hicho.”

Luteni von Pirch na Dk. Buschow pia waliuawa wakiwa juu wa punda wao ambapo majeraha yao yalikuwa makubwa mno. Karibu askari wote wa Kikosi cha 7, Kikosi cha Silaha, Kikosi cha 5 na baadhi ya askari wa Kikosi cha 6 waliuawa kabla hata hawajajua wafanye nini.

Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi pamoja na askari 20 hivi ndio waliofanikiwa kukimbia kutoka eneo hilo la mapigano na kukimbilia upande mwingine wa mlima na kuweka ngome wakijilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahehe. Wapiganaji hao wa wajerumani walijificha kwenye pagala moja la tembe lililokuwa limetelekezwa mlimani. Askari mmoja Msudani ndiye aliyekiona kibanda hicho.

Lakini von Heydebreck aliishuhudia vita hiyo katika kipindi cha dakika mbili au tatu tu kabla ya kupoteza fahamu. “Kulingana na ushuhuda wa Wahehe walioshiriki mapigano yale, vita hivyo havikumalizika mapema kama ambavyo Wazungu wa mstari wa nyuma walivyotegemea, badala yake askari walionusurika waliendelea kupambana hadi saa 4:30 asubuhi na kuwaua maadui wengi (Wahehe).”

Askari wa mwisho wa kikosi cha Luteni von Tettenborn ndio hawakupata madhara makubwa ya mashambulizi ya Wahehe, washukuru kutokana na makosa ya ishara, vinginevyo wote wangeangamia katika kipindi hicho cha dakika 15 tu. Von Tettenborn, Feldwebel Kay na askari kama 20 hivi Wasudani wakahamia upande wa kushoto wa eneo la mapigano na kutengeneza nusu duara kwa ajili ya mashambulizi huku wakiwa wameumia. Wakiwa hapo walipandisha bendera ya Ujerumani juu ya mti na kupiga mbinja ili kuwaita manusura wengine.

Wakati huo Wahehe waliendelea kuwakimbiza manusura na kushambulia kila waliyemuona mbele yao. Mkanganyiko ukaongezeka baada ya kuwasha nyasi.

Mnamo saa 2:30 asubuhi hiyo, Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi wakiwa na askari wao 12 walipenya na kuungana na kikosi cha von Tettenborn. Von Heydebreck alikuwa anavuja sana damu kutokana na majeraha mawili makubwa ya mikuki. Kwa kuwatazama tu watu hao, von Tettenborn akatambua kwamba vikosi vyao vyote vilikuwa vimesambaratishwa na kikosi cha silaha kutekwa, ambapo Mkwawa aliteka bunduki 300. Askari wa jeshi la Wajerumani waliouawa siku hiyo walikuwa zaidi ya 500.

Ilipofika saa 3:00 Luteni Usu Thiedemann, akiwa na majeraha makubwa ya moto aliingizwa kwenye kikosi cha Luteni von Tettenborn akiwa amebebwa na askari waliokuwa wanafanya doria. Nyasi zilizokuwa zinaungua sasa zilimtisha von Tettenborn na manusura wengine.

Hadi kufikia saa 10:00 jioni Luteni von Tettenborn alikuwa amewakusanya majeruhi wengi na kuokota baadhi ya mizigo yao. Wahehe waliokuwa wamepagawa kwa hasira pamoja na moto mkubwa uliokuwa ukiendelea kuteketeza msitu viliifanya kazi ya kuwatafuta majeruhi wengine kuwa ngumu, hivyo wengi waliteketea kwa moto. Von Tettenborn akaamua kuanza kurudi nyuma kabla hajazuiwa na Wahehe.

Wakati wa usiku wa manane kikosi kilichokuwa na Luteni von Tettenborn kikapiga kambi ng’ambo ya pili ya mto tofauti na mahali walipolala kabla ya kuanza mapambano. Kikosi chake sasa kilikuwa na yeye mwenyewe na Luteni von Heydebreck, ma-NCO watatu wa Kijerumani (ingawa Luteni Usu Thiedemann alikufa baadaye njiani), maofisa wawili wa Kiafrika, ma-NCO 62 wa Kiafrika, wapagazi 74 na punda 7. Kutoka hapo wakaanza kutembea hasa nyakati za usiku kurudi nyuma ambapo walifika Myombo Agosti 29.

Hakuna takwimu halisi za idadi ya Wahehe waliokufa kwenye vita hiyo ingawa makadirio ni kati ya 260 hadi 700. Kwa ujumla, Wajerumani walikuwa wameshinda vita dhidi ya wakoloni, ushindi ambao ni wa kihistoria kwa mtawala yeyote wa Kiafrika wakati huo dhidi ya Wazungu. Haya yalikuwa matokeo mabaya zaidi kwenye vita katika historia ya ukoloni wa Wajerumani.

Jeshi la Wahehe halikuwa na haja ya kuhitimisha ushindi wake kwa kuwafuatilia Wajerumani waliosalia ili kuwaangamiza kabisa. Badala yake, kuanzia wakati huo wakaendelea kuishambulia misafara yote ya Wazungu.

WIKI IJAYO:  Harakati baada ya ushindi wa Lugalo

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: