Home > All Stories > Biashara ilivyofuta Utakatifu Ikulu

Biashara ilivyofuta Utakatifu Ikulu

 

 

Na Daniel Mbega

 

SIYO siri kwamba, viongozi wetu wa sasa wa Serikali wamechafuka, wameoza na kuvunda kutokana na kukosa uadilifu na uaminifu. Rushwa imetamalaki kila kona, wengi wametumia na wanaendelea kutumia vyeo vyao, ambavyo ni dhamana, kujilimbikizia mali.

Jinsi wanavyopigana vikumbo kila mahali kuusaka uongozi ni dalili pekee kwamba, huko hawakimbilii kuwaongoza Watanzania, bali kutaka fursa ya kujitajirisha. Wachume hata mahali wasipopanda! Ndivyo wanavyofanya.

Serikali ya awamu hii ndiyo, kihistoria, inaongoza kwa kashfa nyingi za ufisadi, rushwa na uongozi mbovu. Siyo ajabu siku hizi ukipita mitaani ukaambiwa; “Ghorofa lile unaloliona, ni la ‘mheshimiwa’ wa Ikulu ama mwanafamilia wake!” Na hili linatokea kila mji hivi sasa, japokuwa watu hawasemi hadharani, lakini minong’ono imejaa tele.

Enzi za Mwalimu Nyerere, namaanisha katika uongozi wake, hatukuwahi kusikia wala kuona wanafamilia wake – iwe mkewe, watoto ama ndugu zake – wakijihusisha kwenye ujasiriamali wakati Baba wa Taifa akiwa Ikulu. Maadili ya uongozi yalikuwepo.

Awamu ya pili, pamoja na kuwepo kwa kashfa kadhaa, hatukusikia kama zilizofuata, hasa hizi za awamu hii ambazo kwa kweli zinazidi kuichafua Ikulu na kuonekana kama sehemu ya biashara.

Tunaelezwa huku mitaani kwamba, siku hizi hata wageni wanaotaka kuwekeza nchini, wanakwenda moja kwa moja Ikulu, ambako wanaweza kupata fursa kubwa zaidi baada ya viongozi wetu kuzunguka huku na huko ‘kuwakaribisha’ waje wawekeze. Hii ni aibu kubwa.

Kwamba wanafamilia wa Rais Jakaya Kikwete wako kwenye biashara – tena kubwa kubwa – hili siyo jambo geni kwa sababu kila siku tunazisikia taarifa hizi ingawa zimekuwa zikikanushwa kwa nguvu zote. Na kwa vile walio Ikulu wanaonekana kuwa wajasiriamali, basi hata wasaidizi wa Rais, yaani mawaziri na maofisa wengine, nao wameamua kuitafuna nchi wapendavyo, kwa kutumia kofia zao.

Siyo ajabu, baada ya awamu hii kumalizika tukasikia mengi ambayo hatukuyajua, achana na hivi vibilioni vilivyofichwa huko Uswisi. Si kuna waziri mmoja aliwahi kusema Dola milioni moja alizokuwa ameziweka huko ng’ambo ‘vilikuwa vijisenti tu’? Sasa yawezekana hata hizi tulizozisikia ni ‘vijisenti’.

Nakumbuka sana wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi Tanzania mwaka 1995 wanaccm wengi walijitokeza kuwania nafasi hiyo adhimu kwa tiketi ya chama hicho.

Miongoni mwao, ambao nilihudhuria hata mikutano yao ya kutangaza azma zao za kuwania nafasi hiyo walikuwemo mawaziri wakuu watatu wastaafu; Jaji Joseph Sinde Warioba, John Samuel Melecela na Cleopa David Msuya.

Wanaccm wengine walikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho wakati huo Horace Kolimba, Jaji Mark Bomani, Jakaya Mrisho Kikwete, Edward Ngoyayi Lowassa na mgombea ‘asiyefahamika’ wakati huo Benjamin William Mkapa ambaye alikuja dakika za mwisho.

Kuibuka kwa wagombea wengi kiasi hicho ndani ya CCM kuliwafanya Watanzania waamini kwamba ile demokrasia iliyokuwa imefichwa kwa miaka mingi na utawala wa chama kimoja ilikuwa imeibuka na kukomaa. Wananchi sasa waliamini walikuwa na nafasi ya kumchagua mgombea yeyote waliyedhani anafaa badala ya kupewa karatasi ya kura yenye picha ya mtu mmoja na kivuli huku wakilazimika kupiga kura za ‘NDIYO’ au ‘HAPANA’.

Mtanzania wa kijijini kule Malengamakali atajihangaisha vipi kupigia kivuli ambacho hakimuongozi badala ya picha ya mtu ambaye ndiye Chama kimemchagua?!

Lakini pia kuibuka kwa wanaccm wengi kiasi hicho kulimpagawisha sana mtu mmoja; Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliamini hiyo haikuwa demokrasia tena bali chama kilikuwa kimevamiwa na kwamba kilikuwa na viongozi ‘wabaya’, ambao dhahiri aliwaona walikuwa na nguvu na wangeweza kupitishwa na chama kushika madaraka ya nchi.

Pengine kilichomshtua zaidi ni kule kuona Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, John Malecela, ambaye hakuwa amejitokeza mapema kama wenzake, akiibuka ghafla na kupata wadhamini 250,000 waliotakiwa huku akiungwa mkono na kundi kubwa la vijana na baadhi ya wazee.

Akiwa tayari ametajwa mapema kwamba alikuwa anakusudia kumpigia debe mgombea wa upinzani, Mwalimu Nyerere akawaonya wale wabaya ndani ya chama waliokuwa na nguvu, kwamba; “Wasipotupatia mgombea mzuri, hawatutawali… Kama hawatuwekei mgombea mzuri, kwa nini watutawale?”

Nyerere aliona kabisa kwamba chama kilikuwa kimevamiwa na watu wenye fedha, ambao walikuwa tayari kumsimika ‘mtu wao’ kwa kutumia fedha hizo ambazo aliwahi kuziita ‘fedha za bangi’, akimaanisha kwamba zilikuwa fedha chafu ambazo hata upatikanaji wake ulikuwa wa njia zisizo halali ndiyo maana walikuwa tayari kuzitumia watakavyo ili kulinda ‘maslahi’ yao.

Lakini pia inaonekana Nyerere alishtushwa zaidi na kuibuka kwa vijana wawili ambao baadaye walikuja kupachikwa jina la ‘Boys II Men’; Jakaya Kikwete na Edward Lowassa, ambao wakati wa kurejesha fomu za kuwania kuteuliwa kugomea urais kule Dodoma walikodi ndege ya binafsi. Ni huko ambako tunaambiwa Mwalimu aliwahi kuwauliza wagombea, akiwemo Lowassa, ni wapi walikozipata fedha walizokuwa nazo.

Lakini majina yale yalipochujwa na Kamati Kuu ya CCM katika mchakato wa kwanza na kubaki matatu – Msuya, Mkapa na Kikwete – Nyerere alisikika akisema kwamba; “Rais bora angetoka CCM,” na akamtaja Ben Mkapa kwamba ndiye aliyekuwa bora zaidi kati ya wale watatu. Huyu mwingine wa mwisho, Kikwete, akiambiwa ‘kura zake hazikutosha’, hivyo asubiri kipindi kingine.

Mwalimu akamnadi Ben kila pembe ya nchi huku akisema; “Mgombea wa CCM anauzika.” Aliweka matumaini makubwa kwamba mgombea huyo mara atakaposhinda na kutwaa madaraka angeweza kufuata falsafa zake na kujenga taifa lililo imara katika misingi ya haki, usawa, uadilifu na uwajibikaji.

Lakini kabla kampeni rasmi za kitaifa hazijaanza, wanaccm wengi wakatoka na kujiunga na vyama vya upinzani huku baadhi yao, akiwemo Augustine Lyatonga Mrema, wakionekana kuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi.

Mwalimu akasimama kidete kuwaponda wagombea hao huku akitamka bayana; “I can’t let this country to the dogs (Siwezi kuwaachia mbwa nchi hii),” kauli ambayo wapinzani waliiona kama kashfa kwao kufananishwa na mbwa ingawa kihalisia Nyerere hakuwa amemaanisha hivyo.

Nyerere akashika hatamu za kampeni kwa nguvu zote akimpamba na kumsifu ‘mteule’ wake – Mkapa. Kwa kuwa tayari alikuwa amewaponda viongozi wengine wa serikali na chama kama Malecela na Kolimba (R.I.P) kwenye kitabu chake cha ‘Uongozi wetu na hatma ya Tanzania’, aliweza kuzibadili fikra za wananchi wengi ili wamshabikie mgombea wake.

Akawaponda wagombea wengine wa vyama vya upinzani waliokuwa kwenye mchakato huo akisema; “Mnakimbilia Ikulu, Ikulu kuna biashara gani pale? Mnataka kwenda kufanya nini Ikulu? Ikulu ni mahali patakatifu, si mahali pa mchezo mchezo pale. Ni mahali pa kuheshimika!”

Ndiyo. Kauli hizi na nyinginezo alizozitoa Mwalimu ziliwagusa wengi na wakaamini kwamba chaguo lake – Mkapa – lilikuwa sahihi mno. Mkapa, ambaye awali wengi walimkejeli kwamba hajulikani kimataifa tofauti na akina Warioba, Malecela na Msuya, sasa akawa maarufu hata kabla ya kuingia Ikulu.

Hizi ndizo falsafa za Mwalimu Nyerere ambazo zilisaidia Tanganyika ikapata uhuru wake kwa kutumia nguvu ya hoja. Alimudu kuiongoza Tanzania kwa miaka 24 si kwa sababu ya usomi wake na kuzungumza kwake, bali karama ya uongozi ilikuwa ndani yake.

Hata hivyo, kitu pekee ambacho hakukijua ni kwamba, miaka michache baadaye wale aliodhani wangefuata falsafa yake wakawa wamekengeuka na kuamua kuitia najisi Ikulu, sehemu takatifu ambayo Nyerere alipigania kuhakikisha hakiingii ‘kilicho kichafu’.

Yaliyofanyika pale Ikulu na yanayoendelea kufanyika hata le, ambayo kama Nyerere angekuwa hai, hakika angeweza kulia machozi, tena ya damu, kwa kuona kwamba kumbe juhudi zake za kuwapiga vijembe wengine waliotaka kupaendea mahali pale pa juu palipoinuka zilikuwa bure kabisa hasa baada ya wale alioamini wangepaenzi kuamua kuyafanya yale yale aliyokuwa akiyakataza!

Leo hii Watanzania wengi walikuwa wanaombea walau Mwenyezi Mungu angempa uhai zaidi Mwalimu Nyerere wa kuweza “kumuona rais wa awamu ya nne” kama alivyokuwa amesema mwenyewe siku ile ya ‘birthday’ yake ya miaka 75 mwaka 1997, hakika angeweza kushuhudia ufisadi mkubwa ambao ulikuwa unafanywa na wale ambao aliamini wangeyafanya ‘mapenzi ya baba’.

Kilichotokea ni kama ule mfano wa wana wawili, ambapo mkubwa alitumwa na babaye aende shambani, lakini akakataa kwamba hatakwenda, lakini baadaye akabadili mawazo na kwenda. Mdogo akatumwa aende, akasema atakwenda, lakini baadaye hakwenda! Ni nani aliyeyafanya mapenzi ya baba kama si yule wa kwanza?

Mwalimu alikuwa amefanya kazi na wakongwe wengi ambao walijitokeza katika mchakato ule wa mwaka 1995, lakini kwa kuwa huko nyuma walikuwa wamekosea na kuona kwamba hawafai, akaamua kumpigia chapuo ‘mdogo wao’ Mkapa, ambaye ‘alimuahidi’ kwamba angekwenda kutekeleza yale aliyotumwa. Lakini kwa bahati mbaya zaidi, wale wakongwe ambao walikuwa wamekosea huko nyuma walikuwa wamejirekebisha na kuwajibika iwapasavyo, na yule ambaye aliaminiwa kwamba ndiye angeweza kutekeleza mapenzi ya Mwalimu, akafanya ndivyo sivyo.

Mwalimu Nyerere alifariki Oktoba 14, 1999, lakini kwa kudhihirisha kwamba mwanafunzi wake Mkapa alikuwa amemsaliti, tayari alikuwa ameanzisha kampuni ya kibiashara akiwa Ikulu, miezi mitatu na siku 22 kabla Mwalimu hajaaga dunia, yaani Juni 22, 1999 wakati Mkapa na mkewe mama Anna, wakati huo wakiwa madarakani, walipoanzisha kampuni ya ANBEM Limited. Kampuni hiyo ni kifupishi cha majina yao, yaani Anna na Ben Mkapa.

Wakati hayo yakitokea, tayari serikali ilikuwa imeshachafuliwa na kashfa kadhaa za mawaziri wa serikali ya awamu ya tatu, ambapo kwanza Waziri wa Fedha Profesa Simon Mbilinyi na naibu wake Kilontsi Mpologomyi walikuwa wamejiuzulu kutokana na kashfa ya misamaha ya kodi kwa mafuta na minofu ya samaki, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Juma Ngasongwa alikuwa amejiuzulu baada ya kutajwa katika Tume ya Kero ya Rushwa ya Jaji Joseph Warioba kuhusiana na minofu ya samaki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) Dk. Hassy Kitine alikuwa amejiuzulu kwa kashfa ya kumtibia mkewe nje ya nchi kwa mamilioni ya fedha za serikali kinyume cha utaratibu, na naibu waziri wizara ya fedha Monica Mbega alijiuzulu kwa madai ya kwenda kusoma, ingawa wachunguzi wa masuala ya siasa walikuwa wamehusisha kujiuzulu kwake na kashfa ya kuwapeleka ndugu zake kwenye mkutano wa dunia wa vijana jijini Lisbon, Ureno, ambako inasemekana walizamia moja kwa moja.

Tangu hapo viongozi waliokuwa Ikulu ya Tanzania wakaendelea kufanya biashara, tena wakitumia ofisi za serikali, ambapo tunaambiwa kwamba Julai 2002 kampuni ya ANBEM ilichukua mkopo wa Dola za Marekani 500,000 (takribani milioni 620/-) kutoka benki ya NBC, ambayo ilibinafsishwa kwa kuingia ubia na Benki ya ABSA ya Afrika Kusini pamoja na Mwalimu Nyerere, enzi ya uhai wake, kupinga kwa nguvu zote kwamba chombo hicho kisibinafsishwe. Mwezi Desemba ANBEM ikachukua mkopo mwingine wa milioni 250/- kutoka benki ya CRDB.

Miaka miwili baadaye tukashuhudia kuanzishwa ka kampuni nyingine ya Tanpower Resources (ilisajiliwa Desemba 29, 2004), ambayo taarifa za wachunguzi zinabainisha kwamba inamilikiwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa (wakati huo akiwa bado madarakani) na mkewe kupitia kampuni yao ya ANBEM Limited, mtoto wao Nicholas kupitia kampuni yao na mkewe Foster Mbuna iliyoanzishwa mwaka huo huo iitwayo Fosnik Enterprises Limited.

Wengine wanaotajwa kumiliki hisa za Tanpower Resources Company Limited ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini (wakati huo) Daniel Ndhira Yona na mwanawe Danny kupitia kampuni yao ya DEVCONSULT Limited (Yona ana hisa 90% kwenye kampuni hiyo na mwanawe ana 10%), baba mkwe wa Nicholas Mkapa, Joseph Mbuna (R.I.P), kupitia kampuni yake ya Choice Industries Limited, na kampuni ya Universal Technologies Limited inayomilikiwa kwa pamoja na Evans Mapundi na Wilfred Malekia.

Kampuni ya Tanpower Resources ambayo Machi 2006 iliingia mkataba na Tanesco wa kuzalisha umeme wa Megawatts 200 katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 271.8 (takribani bilioni 340/-) mbali ya kuanzishwa na viongozi ambao walikuwa bado wako Ikulu, lakini pia ilikuwa inamilikiwa na familia, au kwa kifupi ni ya ukoo! Tayari Ben Mkapa na mkwewe walikwishagawana kila mtu na chake.

Lakini si hao tu, ziko kashfa nyingi zinazoendelea ndani ya serikali yetu ya sasa na ile iliyopita. Kwa mfano; inakumbukwa jinsi jinsi Benki Kuu ilivyoingia mkenge kwa kulipa mabilioni ya fedha kufidia deni la kampuni iliyoibuka ghafla na kufa ya Meremeta Gold Mine, ambayo ilirithiwa na kampuni ya Tangold.

Tunaambiwa kampuni ya Tangold, ambayo ilisajiliwa Aprili 2005 mjini Port Louis, Mauritius, ilikuwa inamilikiwa na viongozi wakubwa serikalini wakiwemo Gavana wa Benki Kuu Daudi Ballali, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja, Mwanasheria Mkuu wa wa Serikali (wakati huo enzi ya Mkapa) Andrew John Chenge, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Patrick Rutabanzibwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo Vincent Mrisho.

Baada ya Mkapa, Watanzania walikuwa na imani kubwa na uongozi wa Rais Kikwete, ndiyo maana walimpa kura nyingi katika uchaguzi wa mwaka 2005, wakiamini yeye ndiye aliyefaa kuiongoza nchi hii isipokuwa ‘alicheleweshwa’ tu kwa miaka 10.

Lakini ilivyo sasa, wengi wanaona dhahiri mawazo yao hayakuwa sahihi, ikiwa taarifa zinazoenezwa kwamba wanafamilia wake ni wajasiriamali wakubwa wakati yeye akiwa bado Ikulu ni za kweli, na pia wanapoona anashindwa kutoa uamuzi mgumu katika masuala ya msingi yanayolihusu taifa hili.

Kusema ukweli Watanzania hawaielewi serikali hii ambayo inachekelea rasilimali za nchi zinaposombwa na wageni, wao wakiwa hohe hahe, huku viongozi waliokabidhiwa dhamana ya kuzilinda nao wakishiriki kuzisindikiza rasilimali hizo. Ni aibu!

Hakika haya ni matumizi mabaya ya madaraka kwa sababu ni kinyume kabisa na Kanuni za Maadili ya Utawala Bora na Utumishi wa Umma Ibara ya 12 hadi ya 14, na kama Nyerere angalikuwa hai leo akaona namna wapendwa wake, wale aliowateua ‘wanywee kikombe cha bwana wao’, wanavyoyatumia vibaya madaraka yao, kwa kuwapora wananchi mkate wao.

Tuwafananishe na nani viongozi wa zama hizi basi? Tuwafananishe na Mfalme Daudi aliyemtwaa Baarsheba kuwa mkewe kutoka kwa Uria, ambaye aliamua kumuua ili amtwae moja kwa moja? Au tuwafananishe na Mfalme Nebukadneza wa Babeli aliyejitukuza na kujiona kama yuko karibu na Mungu kabla ya kufukuziwa porini kula umande kwa miaka mitatu na nusu kabla ya kutambua kwamba utawala wa wanadamu unawekwa na Mungu?!

Watawala hawa wameonyesha kumkosoa Mwalimu Nyerere kwa vitendo, kwamba kama alidhani Ikulu hakuna biashara, basi wao wameweza kuifanya, tena wakiwa hawana hofu wala woga wa aina yoyote, huku wakisimama majukwaani kusisitiza utawala bora.

Tunataka tuwe na watawala bora, lakini viongozi wa aina hii ambao wanaonekana kuinajisi Ikulu na ofisi za umma hakika wanapandikiza mbegu mbaya kwa vijana wetu, ambao nao wanaendelea kuiga mle mle walimopitia wazee wao na kuzidi kulifanya taifa hili kuwa la watu wasiokuwa makini, ambao ufisadi kwao ni kama kitu kilichohalalishwa.

Laiti kama Nyerere angefufuka leo na kuona jinsi alivyosalitiwa, hakika angeifuta kauli yake kwamba wale aliodhani ‘mbwa’ walikuwa bora zaidi kuliko hawa!

0655-220404

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: