Home > All Stories > Mapato yalikuwa makubwa, lakini wakaubinafsisha Mradi

Mapato yalikuwa makubwa, lakini wakaubinafsisha Mradi

 

 

HUU ni mfululizo wa Ripoti Maalum kuhusiana na mgogoro wa ardhi Kapunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya kama unavyoendelea kusimuliwa na Mwandishi Wetu DANIEL MBEGA, ambaye aliyefanya uchunguzi kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu. Endelea na Sehemu hii ya Saba…

 

MRADI uliokuwa unategemewa kuwa mkombozi wa Taifa katika suala la uzalishaji wa chakula, hasa mpunga, ulidumu kwa miaka mitano tu na baada ya hapo ukayumba na kuporomoka kabisa.

Kwa mfumo wa vigogo wa shirika kuchota kwa mashindano kwenye Mradi wa Mpunga Kapunga, haishangazi kuona hata ripoti za uzalishaji pamoja na mapato na matumizi kuonekana zinakanganya.

Katika msimu wa kwanza wa mradi huo, yaani mwaka 1990/91, eneo lililolimwa lilikuwa hekta 423. Mkanganyiko rasmi unaanzia hapa. Wakati ambapo nyaraka mbalimbali za Serikali, zikiwemo Nyaraka za Zabuni za Kuuza Shamba hilo za Juni 2004, zinaonyesha kwamba katika msimu huo jumla ya tani 1836 zilivunwa ukiwa ni wastani wa tani 4.3 kwa hekta moja, Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi wa Mpunga Kapunga ya Benki ya Maendeleo ya Afrika inaonyesha zilivunwa tani 1,314 za mpunga.

Hii inaonyesha kuwepo na upungufu wa tani 522 za mpunga ambazo haijulikani zilikokwenda, kwani kimsingi Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi ilitegemea zaidi taarifa kutoka serikalini, hususan kwenye Shirika la Nafco lenyewe. Ilikuwaje mpaka maofisa wa ADB wakapewa takwimu zilizo pungufu ni swali ambalo linaweza kujibiwa na wahusika wenyewe.

Lakini tukirejea kwenye Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi, tani 1,314 za mpunga zilipokobolewa zilitoa jumla ya tani 854 za mchele zilizokuwa na thamani ya Sh 123,402,977 (tani moja iliuzwa kwa Sh 144,500).

Gharama zote kwa msimu huo, ikiwemo mishahara na mambo mengine, zilikuwa Sh 98,359,755, hivyo faida kwa msimu wa kwanza ilikuwa Sh 25,014,122.

Kwa msimu wa 1991/92 mkanganyiko pia uliendelea kujitokeza kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo. Nyaraka za Zabuni zinaonyesha kwamba, msimu huo jumla ya hekta 2,550 zililimwa na kutoa mpunga tani 12,240 ikiwa ni wastani wa tani 4.9 kwa hekta moja, lakini kwenye Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi inaonyesha kwamba zilipatikana tani 10,150 za mpunga, ambazo baada ya kukobolewa zilipatikana tani 6,312 za mchele na zilipouzwa kwa bei ya Sh 112,000 kwa tani, zikapatika jumla ya Sh 706,944,000.

Wakati ambapo bei ya mchele ilishuka, mishahara ikaongezeka na kufikia Sh 8,538,748 ukilinganisha na Sh 2,081,599 za mwaka uliotangulia. Haijulikani kama ni kutokana na kuongeza wafanyakazi au nyongeza ya mshahara tu wa Serikali. Gharama za jumla kwa msimu huo zilipanda na kufikia Sh 392,522,872 na kufanya faida ibakie Sh 314,421,128.

Pamoja na eneo la mradi kuongezeka na kufikia hekta 3,000, lakini msimu wa 1992/93 ulikuwa na mapato duni sana huku kisingizio kikiwa mvua kubwa zilizonyesha mwaka huo na kusababisha mafuriko.

Nyaraka za Zabuni zinaonyesha kwamba msimu huo zilipatikana jumla ya tani 5,585 za mpunga ukiwa ni wastani wa tani 1.86 kwa hekta, lakini Ripoti ya ADB/ADF inaonyesha zilizopatikana ni jumla ya tani 5,550 tu ambazo zilipokobolewa zikatoa tani 3,315 za mchele. Lakini bei ya mchele mwaka huo ilipanda sana ambapo tani moja iliuzwa kwa Sh 205,000 na kufanya mapato kuwa Sh 679,575,000. Gharama zote ikiwemo mishahara na mambo mengine zilikuwa Sh 774,201,241, hivyo kuwepo na hasara ya Sh 94,626,241.

Msimu wa 1993/94 nao haukuwa kama ile miwili ya mwanzo, kwani katika eneo la hekta 3,000 zilizolimwa, Nyaraka za Zabuni zinaonyesha kuwa zilipatikana tani 6,831 ukiwa ni wastani wa tani 2.28 kwa hekta, lakini Ripoti ya ADB/ADF inaonyesha tani za mpunga zilizovunwa zilikuwa 5,810 tu na ulipokobolewa ulitoa tani 4,134 za mchele. Bei ya mchele kwa mwaka huo ilikuwa Sh 201,000 kwa tani, hivyo zikapatikana jumla ya Sh 827,575,000. Lakini gharama za uendeshaji ziliendelea kupaa, ambapo safari hii jumla ya gharama zote ilikuwa Sh 1,120,255,824, ikiwa ni zaidi ya Sh 292,297,824 ya mapato halisi. Kwa maana nyingine, msimu huu pia waliendesha kwa hasara.

Ukichungulia kwa undani katika kipindi cha misimu minne utagundua kwamba, taarifa zinakinzana baina ya Nyaraka za Serikali (Zabuni) pamoja na Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi ya ADB/ADF.

Inaonyesha kwamba, jumla ya tani 3,668 za mpunga hazionyeshwi kwenye Ripoti ya Kukamilika kwa Mradi katika kipindi cha misimu minne ukiwa ni upungufu wa tani 522 (msimu wa 1990/91), tani 2,090 (msimu wa 1991/92), tani 35 (msimu wa 1992/93), na tani 1,021 (msimu wa 1993/94).

Hasara hiyo iliendelea hata kwa msimu wa 1994/95 ambapo Ripoti ya ADB/ADF inasema makadirio ya mapato yalikuwa Sh 1,278,340,000 lakini matumizi yakawa Sh 1,349,689,824, hivyo kuwepo na hasara ya Sh 71,349,824.

Katika msimu huo jumla ya tani 9,000 za mpunga zilitarajiwa kuvunwa kwenye eneo la hekta 3,000 zilizolimwa ambapo baada ya kukobolewa zingepatikana tani 5,558 za mchele. Kama ungeuzwa kwa Sh 230,000 kwa tani, basi zingepatikana Sh 1,278,340,000.

Hata hivyo, mapato halisi kwa mujibu wa Nyaraka za Zabuni yalikuwa tani 6,810 za mpunga ukiwa ni wastani wa tani 2.27 kwa hekta moja.

Makadirio kwa msimu wa 1995/96 yanaonyesha kwamba mavuno yangeanza kupanda tena, kwa mujibu wa Ripoti ya ADB iliyotokana na nyaraka mbalimbali walizozipata kwenye mradi ikiwemo Ripoti ya Nyongeza kwa Watumishi (SAR). Eneo lililolimwa lilikuwa la hekta 3,000 na mavuno yalitarajiwa kuwa tani 10,500 za mpunga. Baada ya kukobolewa ungetoa tani 5,532 za mchele, zikiwa chache kuliko za msimu uliotangulia. Mchele huo kama ungeuzwa kwa Sh 271,400 kwa tani, zingepatikana Sh 1,773,056,200 ambapo baada ya kutoa gharama za matumizi Sh 1,538,484,804 Mradi ungebakiwa na faida ya Sh 234,571,396. Nini kilichosababisha gharama kuongezeka na mradi kuendeshwa kwa hasara katika kipindi cha miaka mitatu, nadhani wahusika ndio wanaojua.

Hata hivyo, kwa msimu wa 1996/97, mavuno yalitarajiwa kuongezeka zaidi na kufikia tani 12,000 za mpunga ambazo baada ya kukobolewa zingetoa tani 7,900 za mchele. Kwa kuwa wakati huo tani moja iliuzwa Sh 320,252, jumla ya fedha ambazo zingepatikana zingekuwa Sh 2,497,365,500. Gharama zote zilikuwa Sh 1,761,262,880, ambapo faida ilingekuwa Sh 736,702,719.60.

Msimu wa 1997/98 walipanga kuvuna tani 13,500 za mpunga ambazo zingetoa tani 8,483 za mchele. Wakati huo tani moja ya mchele iliuzwa kwa Sh 377,891, hivyo zingepatikana jumla ya Sh 3,205,703,304.88. Matumizi ya jumla nayo yakaongezeka msimu huo na kuwa Sh 2,024,141,010, hivyo faida ilitarajiwa kuwa Sh 1,181,562,294.88.

Msimu wa 1998/99 zilitarajiwa kulimwa jumla ya hekta 3,000 na mavuno yalitarajiwa kuwa tani 13,500 za mpunga ambazo zingetoa mchele tani 8,483 na kama zingeuzwa kwa Sh 445,919 zingepatikana jumla ya Sh 3,782,728,892.76 ambapo gharama zote zilitarajiwa kuwa Sh 2,284,701,604.13, hivyo faida ingekuwa Sh 1,398,028,295.63.

Makadirio ya msimu wa 1999/2000 yalikuwa kulima ekari 3,000 ambazo zingezalisha tani 13,500 pia za mpunga ambazo zingetoa tani 8,483 za mchele. Ikiwa zingeuzwa kwa Sh 526,184 kwa tani zingepatikana jumla ya Sh 4,463,621,281.71. Gharama zilitarajiwa kuwa Sh 2,749,474,002.56, kwa maana hiyo faida ingekuwa Sh 1,714,147,279.16.

Makadirio hayo yaliwekwa mpaka msimu wa 2009/2010 kama shamba hilo lisingebinafsishwa, ambapo mavuno kwa msimu huo yangekuwa tani 13,500 za mpunga ambazo zingetoa tani 8,483 za mchele. Kwa mwaka 2010, kama tani moja ya mchele ingeuzwa Sh 1,420,463, basi zingepatikana jumla ya Sh 12,049,787,369. Kwa makadirio, gharama za jumla zingekuwa Sh 9,548,571,545.10, hivyo Madi huo wa Kapunga ungetengeneza faida ya Sh 2,501,215,823.48.

Kwa muktadha huo, inaonekana kabisa Mradi wa Mpunga Kapunga ungeweza kuwa na tija, siyo ya kuzalisha chakula kwa wingi tu, bali hata kutengeneza faida kubwa na kuwezesha kujiendesha kwa miaka mingi kama si usimamizi mbovu pamoja na kisingizio cha ubinafsishaji.

FUATILIA: Mchakato wa kulibinafsisha Shamba la Kapunga waanza

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: