Home > All Stories > Tusipoangalia tutaibinafsisha Serikali

Tusipoangalia tutaibinafsisha Serikali

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye utawala wake ndio unaotajwa kutekeleza ‘kwa vitendo’ sera ya ubinafsishaji.

 

Na Daniel Mbega

 

BADO najiuliza bila kupata jibu sahihi kuhusiana na Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma ya mwaka 1992 ambayo ilishuhudia mabadiliko katika mashirika 400 yaliyogawanywa katika makundi matatu makuu – mashirika ya biashara; mashirika ya huduma za kawaida; na mashirika ya huduma nyeti.

Ni kweli kwamba, mengi kati ya mashirika hayo yalikuwa yakiendeshwa kwa ruzuku kutoka serikalini, ambapo kwa mujibu wa taarifa ni kwamba, kila mwaka serikali ilikuwa inatumia Sh 100 bilioni kwa ajili ya mashirika hayo.

Tulisadikishwa kwamba, ubinafsishaji huo ungeyakomboa mashirika hayo ya umma ambayo mengi yalikuwa yakiendeshwa kwa hasara licha ya kufanya uzalishaji. Hapa pia tunaambiwa kuwa yalikuwa yakiingiza hasara ya Sh 300 bilioni kwa mwaka!

Athari zilizoambatana na zoezi hilo zilikuwa nyingi, lakini kubwa zaidi ni kwamba, wafanyakazi wengi walipunguzwa kazi, wakapunjwa mafao yao na wengine mpaka sasa mashauri yao bado yangali mahakamani wakipinga kiwango cha mafao waliyopewa.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, zoezi la ubinafsishaji lilifanywa kwa misingi mibovu ya kuwafurahisha wakubwa hasa IMF, Benki ya Dunia na Paris Club huku wakiiweka Tanzania miongoni mwa kundi la nchi zenye madeni makubwa yasiyolipika. Wakawahadaa viongozi wetu kwamba kwa kuridhia Sera ya Ubinafsishaji, wangefutiwa madeni na kupunguziwa mzigo mkubwa uliokuwa ukiikabili nchi yetu.

Sera hiyo iliyotangazwa wakati huo kwamba ni ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikalenga kuindoa serikali katika uendeshaji wa mashirika yasiyo na tija, hivyo mojawapo ua mikakati ikawa kuyauza kabisa, kuingia ubia ama kuuza baadhi ya rasilimali zake.

Kinachowaumiza akili Watanzania walio wengi ni kwamba, hao wawekezaji walioingia ubia ama kubinafsishiwa mashirika na kampuni hizo za umma, wengi wao walikuja mikono mitupu, wakatumia rasilimali hizo walizozikuta, ambazo ni za Watanzania, kuomba mikopo ya mabilioni ya fedha kwenye taasisi za fedha, tena za ndani!

Mbaya zaidi ni kwamba, viongozi wetu wakabinafsisha hata mashirika yale ambayo yalionekana kuwa na faida. Miongoni mwake ni Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kampuni ya Sigara (TCC) pamoja na mashamba yetu ya kilimo yaliyokuwa chini ya Shirika la Kilimo na Chakula (Nafco). Hapa hata mwendawazimu anatucheka.

Najaribu kujiuliza; kama mashirika hayo yalikuwa yakiingiza hasara, hivi walijiuliza hasara hiyo ilitokana na nini? Tulikuwa na malighafi ya kutosha, fursa ya masoko ya ndani ilikuwepo kubwa (kama isingekuwepo tusingekuwa na haja ya kuagiza bidhaa kutoka nje), wataalamu walikuwepo lakini hawakutumiwa vyema. Tatizo kubwa lililokuwepo ni uongozi mbovu wa hao watumishi wa umma ambao waligeuka mchwa na kuyatafuna mashirika hayo.

Halafu kilichotokea ni kwamba, wengi kati ya hao waliokuwa wakiyaongoza awali ndio waliokula njama za ‘kujibinafsishia’ mashirika hayo mara waliposikia kuna Sera hiyo, hivyo walifanya makusudi kuyaua.

Nakumbuka mwezi Aprili 2012, katika mahojiano na Kigoda cha Mwalimu, Rais mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akihojiwa na Mwenyekiti wa Kigoda hicho Profesa Issa Shirvji, aling’aka kwamba hakufanya makosa kuyabinafsisha mashirika hayo wala asilaumiwe kutokana na kutokuwa na ufanisi baada ya kubinafsishwa.

Ikiwa mashirika haya yalikuwa yanaendeshwa kwa hasara na serikali ilikuwa ikitoa ruzuku, mbona hivi sasa serikali hiyo hiyo inatoa ruzuku kwa vyama vya siasa ambavyo kimsingi havizalishi? Kama ilikuwa na dhamira nzuri, basi serikali ingeangalia matatizo yaliyokuwepo kwenye mashirika hayo na kuyatatua, vinginevyo zoezi hili liliharakishwa kwa faida ya wachache.

Tumeshuhudia jinsi viongozi wetu, akiwemo Mkapa mwenyewe, walivyojibinafsishia baadhi ya mashirika ya umma wakati wakiwa madarakani. Hii inatoa picha halisi kwamba, wengi walilifurahia zoezi hilo kwa sababu walinufaika nalo, kwani mashirika mengi yaliuzwa kwa bei ya kutupa kuliko thamani halisi.

Ni kutokana na mukhtadha huo ndiyo maana ninasema ipo siku tunaweza tukafikia hatua ya ‘kuibinafsisha’ hata serikali yetu. Kama tulikubali vitisho vya wakubwa IMF na WB tukaua mashirika na kampuni zetu za umma, siyo ajabu utafika wakati wakubwa hao hao, kwa kutumia visingizio vya ufadhili na madeni tuliyolimbikiza, wakatuletea sera nyingine ambayo itasababisha serikali iingie kwenye ubia.

Hili nadhani limeanza kujitokeza, kwa sababu kitendo cha kubinafsisha njia za usafirishaji kama Reli ni mojawapo ya hatua mbovu ambazo nchi inaweza kuingia. Miundombinu ya usafirishaji ni mojawapo ya masuala ya kiusalama zaidi ambayo hayapaswi kuwa chini ya mbia wala mwekezaji.

Tumeshuhudia katika Shirika la Reli Tanzania (TRC – sasa TRL) ambalo tuliwapangisha Wahindi. Badala ya kuboresha huduma wakaanza kwa kuleta mabehewa na injini mbovu zilizopakwa rangi na kuifanya nchi yetu kama jalala, wakasitisha safari katika baadhi ya njia zilizokuwa zikitumika kama Reli ya Moshi, Reli ya Kidatu na kadhalika. Hali ikawa mbaya zaidi ya ilivyokuwa kabla ya wawekezaji hao kuingia.

Ni mara ngapi serikali ilitoa mabilioni ya fedha kulipa mishahara ya wafanyakazi waliokuwa wanagoma? Halafu wawekezaji hao hao wakawa wanasubiria mkopo kutoka Benki ya Dunia ili kuikarabati Reli ya Kati, kazi ambayo hata serikali yetu ingeweza kuifanya bila matatizo.

Sasa kuna mpango wa kuibinafsisha bandari, halafu vitakuja viwanja vya ndege. Lakini madhara yake tumeyaona kwa sababu Twiga hai wamesafirishwa kupelekwa ughaibuni huku wenye dhamana ya uongozi wakichekelea.

Tunaona suala la uwekezaji katika kilimo linavyoshika kasi huku viongozi wetu wakiendelea kuwahamasisha wageni kuja kutwaa ardhi. Watawala wenyewe tunaambiwa wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi nchini, mpaka visiwa na mambo mengine kadha wa kadha.

Wanajamii wenzangu, lazima tutambue kwamba, tunapobinafsisha rasilimali nyeti kama ardhi, matatizo yake yatakuwa makubwa kiusalama, kwa sababu utafika wakati ambapo sehemu kubwa ya ardhi itakuwa inamilikiwa na walowezi huku Watanzania walio wengi wakiwa hawana kitu.

Kwa msingi huo, walowezi hao wanaotuhadaa kwamba wanakuja kuendesha kilimo kikubwa, watawafanya Watanzania kuwa watwana kama ambavyo tumeshuhudia katika mataifa mengine kama Zimbabwe na Afrika Kusini.

Kwanza hata waliobinafsishiwa yaliyokuwa mashamba ya umma tumeona kwamba wamechukua mikopo kwa kutumia mashamba yetu hayo hayo, halafu wameshindwa kutimiza masharti walau hata kwa kufikia nusu ya uzalishaji uliokusudiwa, tofauti na nyakati ambazo serikali ilikuwa ikiyamiliki.

Ndiyo, watu wanasema ubinafsishaji umekuwa wa mafanikio na tunashuhudia uzalishaji kwenye viwanda vya sukari ukipaa, lakini si hawa hawa ndio wanaopandisha bei ya sukari kila siku? Ni mchezo gani mchafu ambao wanaufanya kwa kuficha sukari ili iadimike, waagize nje kwa gharama nafuu halafu waichanganye na waliyozalisha ili wauze kwa bei ya juu zaidi?

Nadhani kuna haja ya watunga sera wetu kuyaangalia mambo haya kwa makini, wasijifikirie wao tu, bali wafikirie vizazi vyetu vijavyo. Tusingependa kuona wanaibuka akina Chifu Mazengo na Chifu Mkwawa wapya kuanza kuipigania ardhi yao.

Ni ushauri tu, ndugu zangu, wala msinichukie.

 

0655-220404

 

Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: