Home > All Stories > MWALIMU NYERERE, WENZIO WANAUVUNJA MUUNGANO!

MWALIMU NYERERE, WENZIO WANAUVUNJA MUUNGANO!

Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume

Na DANIEL MBEGA

Salaam Mwalimu Nyerere,
Sina shaka kwamba huko uliko umepumzika kwa amani, kwa uwezo wa Mungu. Yawezekana umekuwa mwenyeji huko na kazi yako njema uliyoifanya katika kuhakikisha Tanganyika inajitawala, na hatimaye inaungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuzaa Tanzania, bado ni kitambulisho tosha ndiyo maana leo hii, miaka 14 baada ya kifo chako, bado Watanzania tunakukumbuka huku duniani.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea huku Tanzania. Kwa kifupi, mambo yameharibika. Natamani waraka wangu ungekufikia mwenyewe mkononi ili nikukumbushe ama nikupashe yanayoendelea huku.
Wale wote uliowanadi mwaka 1995 ili waienzi Ikulu yetu, walikugeuka miezi michache tu baada ya wewe kulala na babu zako. Wakaigeuza Ikulu kuwa sehemu ya biashara – ingawa wapo wengine uliwauliza “…Mnakimbilia Ikulu kufanya biashara gani!” Viwanda vyote ulivyopigania kuanzishwa waauziana wenyewe. Ikulu ikawa sehemu ya kusaini mikataba mibovu ambayo immeshuhudia madini yetu yalikuvunwa na kupelekwa nje huku sisi tukibaki na mashimo tu.
Kwa kifupi, uliona wanafaa walikusailiti. Maadili ya uongozi uliyoyasisitiza yakatoweka. Vita ya rushwa imeshindikana kwani wenye dhamana ya kupambana nayo ndio vinara wa kutoa na kupokea rushwa. Natamani hata Chifu Fundikira angekuwepo naye aone wenzake wanavyofaidi – pengine angesikitika kwa nini yeye aliondolewa kwenye Baraza lako la Mawaziri miaka michache tu baada ya uhuru.
Ufisadi umetamalaki kila kona, chaguzi zimegubikwa na rushwa mbaya. Chama chako cha Mapinduzi kimekuwa ‘Chama cha Matajiri’. Bora hili ni neon zuri, lakini wengine wanakiita ‘Chama cha Mafisadi’, au ‘Chama cha Majangili’ na wengine wanathubutu kusema ni ‘Chama cha Majambazi’, ilimradi kila mmoja anatamka neno analoona linafaa. Maskini hawana nafasi, wachache tu ndio wana sauti kwa sababu ya fedha zao.
Wale uliowapinga ndani ya Chama wakati ule, uliowahoji kuhusu walikopata utajiri wao, leo hii ndio wanaoabudiwa. Mbaya zaidi wanapita mpaka misikitini na makanisani kutoa misaada, halafu wanapigiwa makofi na kuimbiwa mapambio. Ungewaona, nina imani ungemwaga machozi. Naamini mama yetu Maria anaugulia moyoni kwa yanayotokea.
Mwalimu, sikuwepo wakati huo, lakini nakumbuka ilikuwa Jumapili, Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati wewe – ukiwa Mwenyekiti wa TANU – ulipokutana na Mwenyekiti wa Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid Amani Karume mjini Dar es Salaam na kusaini hati ya makubaliano ya kuziunganisha nchi zenu. Muungano huu ulifikiriwa kwa takribani miezi mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika mapinduzi ya kuung’oa utawala dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar Januari 12, 1964. Kabla ya kutiwa saini, nyote wawili mlikuwa mmefanya mazungumzo mara kadhaa mjini Dar es Salaam na Unguja na ndipo mkafikia mwafaka wa kuziunganisha nchi hizo.
Wapo walioupinga wakati huo (na wanaendelea kuupinga) kwamba haukufuata misingi inayotakiwa katika muungano halisi, lakini pia wapo walioufurahia na wanaendelea kuufurahia kwa kuwa umeleta udugu na kujenga umoja na mshikamano.
Mwalimu, imebaki miezi michache tu ili Muungano huu utimize miaka 50, lakini nina mashaka kama hautakufa kabla ya miaka hiyo kutimia. Umoja, amani, upendo na mshikamano uliojengwa na muungano huo umetoweka kabisa.
Advertisements
Categories: All Stories
  1. No comments yet.
  1. No trackbacks yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: